Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ramaphosa: Vurugu na ghasia zilipangwa

33d7cff636197e49a50f09331ad49336 Ramaphosa: Vurugu na ghasia zilipangwa

Sun, 18 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema vurugu na ghasia zilizotokea nchini humo kwa takribani wiki nzima mfululizo zilipangwa na kueleza kuwa, kitendo hicho ni uvurugaji wa demokrasia.

Vuruguzi hizo ziliibuka saa chache baada ya Rais wa zamani wa taifa hilo, Jacob Zuma kufungwa jela miezi 15 kwa kosa la kuidharau Mahakama.

Tangu kuanza kwa vurugu hizo idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka na kufikia 212 kwa mujibu wa serikali nchini humo.

Maofisa wa Polisi wamekuwa wakilinda bidhaa za chakula zilizokuwa zikiwasili kwenye maduka makubwa kutokana na vitendo vya uhalifu na wizi kwenye maduka hayo vilivyofanyika tangu vurugu zianze.

Inakadiriwa bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni moja zimeibiwa katika mji wa KwaZulu-Natal katika maduka takribani 800 yaliyovamiwa na waandamanaji.

“Ni wazi kuwa haya matukio ya vurugu na maandamano yalishapangwa. Kuna watu waliyaratibu kabisa,” alisema Ramaphosa alipotembelea mji wa KwaZulu-Natal kuangalia hali ya uharibifu wa mali na vifo vya watu.

Alisema vuruguzi hizo ni mbinu ya kuvurugu demokrasia ya muda mrefu nchini Afrika Kusini na kueleza kuwa tayari wahusika wamefahamika bila kufafanua zaidi.

Katika mji wa KwaZulu-Natal, idadi kubwa ya watu imeonekana ikipanga mstari kutaka chakula hasa nyakati za asubuhi.

Kwa mujibu wa watu waliozungumza na vyombo vya habari, watu wamekuwa wakinunua vyakula na vifaa muhimu kutokana na wasiwasi walionao kuhusu upatikanaji wa bidhaa hizo hapo baadaye.

Kutokana na wiki nzima ya maandamano na vurugu, imesababisha barabara kuharibiwa vibaya na nyingine kuzibwa kabisa na hivyo kuwa kikwazo kwa usambazaji wa chakula katika maeneo mbalimbali.

Wanajeshi wamesambazwa katika maeneo mbalimbali muhimu, huku polisi wakifanya doria na kusindikiza magari yaliyobeba vifaa kama mashine za kupumulia, dawa na vitu vingine muhimu kwa mahitaji maalumu.

Akizungumza kwa muda wa dakika 30 kwenye hotuba yake aliyoitoa jana, Rais Ramaphosa alisema hakuna uhaba wa chakula na kuwataka wananchi waondokane na wasiwasi wa kununua bidhaa nyingi kwa wakati mmoja.

Alisema takribani watu 2,500 wamekamatwa na Polisi wakihusishwa na vuruguzi hizo.

“Nawaomba tuwe kitu kimoja, tuache vurugu kwani hazitasaidia nchi hii kuendelea. Tupo katika mapambano ya kulinda demokrasia, maisha na Katiba yetu lakini kubwa zaidi kulinda usalama wetu. Hii ni vita ambayo lazima tushinde,” alisema Rais Ramaphosa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz