Polisi wa Kiislamu katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria wametumwa misikitini ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, jeshi la polisi la kidini, linalojulikana kama Hisbah Board, lilionya kwamba wale wanaojihusisha na maovu ya kijamii katika mwezi huo mtakatifu wataadhibiwa, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
"Baadhi ya vijana wanaokula hadharani wakati wa mfungo pia hawatasalimika," kamanda mkuu wa bodi hiyo, Harun Ibn-Sina, alinukuliwa akisema.
Bw Ibn-Sina alitoa wito kwa Waislamu kuwasaidia mayatima na wahitaji katika kipindi cha mfungo kilichoanza Alhamisi.
Bodi ya Hisbah inatekeleza sheria za Kiislamu huko Kano, jimbo lenye Waislamu wengi.