Polisi nchini Mauritania imemtia mbaroni Rais wa zamani wa nchi hiyo Mohamed Ould Abdelaziz huku kikao cha kesi yake kikitazamiwa kufanyika. Rais huyo wa zamani wa Mauritania anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mamlaka na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria. Hayo yameelezwa na wakili wake.
Mohamed Ould Abdelaziz aliye na umri wa miaka 66 awali aliagizwa kuripoti kituo cha polisi hata hivyo alikataa. Mawakili wanaomtetea wameeleza kuwa, polisi walifika nyumbani kwa rais huyo wa zamani wa Mauritania katika mji mkuu Nouakchott wakiwa na waranti wa kumtia nguvuni na kisha walimkamata.
Kikao cha nadra cha kusikiliza kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Mauritania kilitazamiwa kuanza leo asubuhi; ambapo Abdelaziz alisalia korokoroni jana usiku.
Shakhsia wengine kadhaa wa wakati wa utawala wa Rais Ould ambao wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi, kutakatisha pesa na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria wametiwa nguvuni.
Jenerali huyo mstaafu aliingia madarakani nchini Mauritania kufuatia mapinduzi na alisalia mamlakani kwa miaka 11. Mohamed Ould Abdelaziz alijizulu mwaka 2019 baada ya kumalizika mihula yake ya miwili ya urais.
Baada ya kuondoka madarakani Mohamed Abdelaziz, Mohamed Ould Ghazouani ndiye aliyeshika hatamu za kuiongoza Mauritania katika makabidhiano ya kwanza ya madaraka kati ya viongozi waliochaguliwa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo iliyoathiriwa na mapinduzi kadhaa ya kijeshi na uasi.