Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Zimbabwe asema ameshinda kwa njia ya haki

Rais Zimbabwee.jpeg Rais wa Zimbabwe asema ameshinda kwa njia ya haki

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais mteule wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametupilia mbali ripoti za baadhi ya waangalizi wa kimataifa waliopinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Mnangagwa alikuwa akitoa hotuba yake ya kusherehekea Ikulu Jumapili na kusema kwamba alishinda uchaguzi kwa haki na hatakengeushwa na maoni mengine.

Ameongeza kuwa, "Ninafahamu kuwa baadhi ya wajumbe wa waangalizi walivuka wajibu wao na kuanza kuhoji sheria iliyopitishwa na bunge letu. Ni maoni yangu kwamba kila nchi huru inapitisha sheria yake kupitia bunge lao na Zimbabwe pia ilifanya hivyo." Aidha amesema hakusimamia uchaguzi bali alishiriki kama mshindani na kuongeza kuwa: "Nina furaha kwamba nilishinda uchaguzi."

Mnangagwa aliwashukuru wananchi kumchagua tena kuhudumu kama Rais wa Zimbabwe.

"Kuna kazi kubwa zaidi ya kufanya. Kwa pamoja, kama watu wamoja tulioungana tutaendelea na msururu wa ustawi ulioshuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hakuna mtu na hakuna mahali patakapoachwa nyuma".

Aidha ametoa wito wa kuwepo amani baada ya uchaguzi.

"Hadi sasa, tumewaaibisha maadui waliotamani kuona tukiwa tumegawanyika na katika machafuko. Tutabaki kuwa watu wa umoja, wapenda amani na wastahimilivu, kuanzia Zambezi hadi Limpopo, Plumtree hadi Mutare, tukiimba wimbo mmoja wa taifa kwa fahari, chini ya wimbo mmoja na bendera ya taifa."

Aidha amesema: "Wazimbabwe wenzangu; Katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi tunachoingia sasa, tuendelee kuwa macho na tulinde kwa wivu mazingira yaliyopo ya amani na utulivu. Kinachotuunganisha ni kikubwa zaidi kuliko kile ambacho kinaweza kutugawa."

Mnangagwa ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 52 ya kura dhidi ya wagombea wengine 10 akiwemo mpinzani wake mkuu, kiongozi wa Chama cha Wananchi (CCC) Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44 ya kura.

Chamisa amesema upinzani utaunda serikali mpya, bila kutoa maelezo. Hakujibu maswali iwapo chama chake kitapinga matokeo hayo mahakamani.

Chamisa amewaambia waandishi wa habari na maafisa wa chama kwamba. “Hatutasubiri kwa miaka mitano. Lazima kuwe na mabadiliko sasa."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live