Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Senegal aitaka Ulaya kusaidia kukabili ugaidi eneo la Sahel

Rais Wa Senegal Aitaka Ulaya Kusaidia Kukabili Ugaidi Eneo La Sahel.png Rais wa Senegal aitaka Ulaya kusaidia kukabili ugaidi eneo la Sahel

Fri, 30 Aug 2024 Chanzo: Bbc

Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye ameitaka Ulaya kusaidia kukabiliana na tishio la usalama linaloongezeka huko Sahel, eneo tete ambalo limekabiliwa na mfululizo wa mashambulizi mabaya katika siku chache zilizopita.

Ametoa wito huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, ambaye alikuwa anamaliza ziara yake Afrika Magharibi.

"Hali katika eneo la Sahel inataka uhamasishaji wa kimataifa wa jumuiya ya kimataifa," alisema Rais Faye, ambaye pia anahudumu kama mwezeshaji katika juhudi za ECOWAS kurejesha Mali, Niger, na Burkina Faso katika umoja huo. Alisisitiza haja ya Ulaya kuzidisha uungaji mkono wake kwa Sahel, ikizingatiwa kwamba "Afrika na Ulaya zina hatima iliyounganishwa ya usalama."

Ombi lake linawadia siku chache baada ya Burkina Faso kushuhudia moja ya mashambulizi yake mabaya zaidi.

Makumi ya raia na vikosi vya usalama waliuawa na wanamgambo katika eneo la Kaskazini la Barsalogho mnamo Agosti 24.

Kundi la wanajihadi lenye uhusiano na Al-Qaeda, Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lilidai kuhusika na shambulio hilo la kikatili, ripoti zikidokeza kuwa watu 200 waliuawa kwa jumla wakati wakichimba mitaro ili kulinda kijiji chao dhidi ya wanamgambo.

Mamlaka za Burkina Faso, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, EU, Marekani na hata ECOWAS walilaani shambulio hilo.

Bado haifahamiki jinsi Burkina Faso, Mali, na Niger zitatafsiri wito wa kiongozi wa Senegal wa kuingilia kati kwa Ulaya katika mgogoro wa Sahel, kwani walivunja uhusiano na vikosi vya Magharibi na kuwaamuru watoke katika eneo hilo hilo la Sahel wakati bado hali ikiwa tete.

Nchi hizo tatu ziliunda muungano wa kijeshi ili kukabiliana na uasi na kuendelea kuwa na uhusisano wa kiusalama na Urusi ambayo huwapa silaha na wale inaowaita kama "wakufunzi wa kijeshi."

Chanzo: Bbc