Rais wa Niger Mohamed Bazoum amepongeza maendeleo katika kupambana na Boko Haram na wapiganaji wa kundi la Islamic State West Africa Province akisema wanashinda vita hivi.
Bazoum alikuwa akizungumza wakati wa ziara yake kusini-mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Nigeria.
“Amesema wanashinda vita hivyo na inabidi waongeze juhudi kidogo ili kukamilisha kazi yote, akiwa anazungumza na wanajeshi walioko katika mji wa Gueskerou aliongeza kuwa mwisho wa Boko Haram upo karibu sana”.
Lakini kulingana na mwanasiasa kutoka jimbo hilo Boko Haram wanaendelea kusambaza hofu kwa kuwanyanyasa watu kwa utekaji nyara, kushinikiza wengine kukimbia vijiji vyao kwa mara nyingine tena.
Eneo linalozunguka Diffa ni makazi ya wakimbizi 300,000 wa Nigeria na watu waliokoseshwa makazi ndani ya nchi kutokana na unyanyasaji wa Boko Haram na Islamic State West Africa Province, kulingana na UN.
Kampeni ya kijeshi ya Niger dhidi ya makundi ya kijihadi inaendelea sehemu kubwa ikijikita katika mipaka ya nchi hiyo na Mali na Burkina Faso.