Rais aliyepinduliwa wa Niger ameonekana kwa mara ya kwanza tangu jeshi lilipomzuilia baada ya kufanya mapinduzi wiki iliyopita.
Mohamed Bazoum alikutana na kiongozi wa Chad Mahamat Idriss Déby Itno katika mji mkuu wa Niger, Niamey.
Bw Déby anaongoza juhudi za upatanishi ili kumaliza mzozo huo baada ya viongozi wa Afrika Magharibi kuwapa wanajeshi makataa ya siku saba kuacha madaraka au kuhatarisha hatua za kijeshi.
Pia alikutana na mkuu wa kikosi cha Ulinzi wa rais aliyejitangaza kuwa kiongozi mpya wa nchi.
Jenerali Abdourahmane Tchiani, mkuu wa kitengo cha walinzi wa rais, alijitangaza kuwa mtawala mpya wa Niger siku ya Ijumaa.
Bw Déby alisema juhudi zake za upatanishi zililenga kutafuta "suluhisho la amani la mgogoro ambao unatikisa" Niger, ambayo inapakana na Chad.
Hakutoa maelezo zaidi, lakini ofisi yake ilitoa picha yake akiwa ameketi karibu na Bw Bazoum anayetabasamu.
Alitumwa nchini Niger na viongozi wa jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, ambao walisema Jumapili kwamba serikali ya kijeshi ina wiki moja kurudisha mamlaka kwa rais aliyechaguliwa.
Umoja wa kikanda "utachukua hatua zote muhimu kurejesha utulivu wa kikatiba" ikiwa matakwa yake hayangetekelezwa.