Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Mauritania achukua rasmi nafasi ya mwenyekiti wa zamu wa AU

Maurtania Raissss.jpeg Rais wa Mauritania achukua rasmi nafasi ya mwenyekiti wa zamu wa AU

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Mauritania amechukua rasmi wadhifa wa mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika (AU) katika ufunguzi wa Mkutano wa 37 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa umoja huo huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Jana Jumamosi, Rais Mohamed Ould Cheikh Ghazouani alichukua nafasi ya mwenyekiti anayemaliza muda wake yaani Rais Azali Assoumani wa Comoro, ambaye alichukua uenyekiti wa AU mwezi Februari mwaka jana katika kikao cha 36 cha bunge la umoja huo.

Katika hotuba yake ya kupokea rasmi wadhifa huo, Rais wa Mauritania amesisitizia haja ya kuheshimiwa na kufanikishwa kivitendo matarajio ya jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Afrika, hasa uhuru wa kijamii na kiuchumi wa Afrika pamoja na umoja na ustawi wake.

Katika sehemu moja ya hotuba yake, Rais Ghazouani amesema: "Ninashukuru sana kwa kupewa heshima hii na ninaelewa wingi wa majukumu niliyo nayo, hasa katika kipindi hiki kigumu."

Picha ya pamoja ya viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia

Wakati wa uenyekiti wake, Rais Assoumani wa Comoro aliangazia masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha utulivu na maendeleo yanapatikana barani Afrika, kuinua nafasi ya AU na ya bara la Afrika kwa ujumla katika ngazi za kimataifa, pamoja na mageuzi ya jumuiya hiyo yenye wanachama 55.

Mkutano wa kilele wa siku mbili wa AU unafanyika chini ya kaulimbiu ya mwaka 2024 ambayo ni: "Elimisha Mwafrika anayefaa kwa Karne ya 21: Kujenga mifumo thabiti ya elimu kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mafunzo jumuishi, ya kudumu, bora na yanayofaa barani Afrika."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live