Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Madagascar aanza muhula mpya wa uongozi

Rais Wa Madagascar Aanza .jpeg Rais wa Madagascar aanza muhula mpya wa uongozi

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Andry Rajoelina ataapishwa kwa muhula mpya kama kiongozi wa Madagascar leo Jumamosi wakati upinzani ukisusia kushiriki sherehe za kuapishwa kwake na wasiwasi wa kimataifa ukiongezeka kuhusu mustakabali wa kisiasa wa kisiwa hicho.

Sherehe hizo zitafanyika katika uwanja mkubwa zaidi wa Madagascar na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka mataifa mengine ya Afrika.

Lakini marais wawili wa zamani, Marc Ravalomanana na Hery Rajaonarimampianina, ambao walihudhuria kuapishwa kwa Rajoelina mnamo 2018, mwaka huu hawatadhuria sherehe hizo.

Wao ni sehemu ya muungano wa upinzani ambao ulifanya karibuni maandamano ya kila siku kwa wiki kadhaa kabla ya kufanyika kura ya Novemba 16 kulaani kile walichokiita "mapinduzi ya kikatiba" ya rais kwa ajili ya kuendelea kubakia madarakani.

Maandamano yamepigwa marufuku mjini Antananarivo tangu Jumanne.

Baada ya uchaguzi, wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine wafadhili wakuu walielezea wasiwasi wao kuhusiana na mivutano na matukio yaliyotawala wakati wa kampeni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa waangalizi wa ndani na wa kimataifa wa uchaguzi, walibaini kuwepo kasoro katika mchakato wa uchaguzi.

Mataifa ya Magharibi yalisema katika taarifa ya pamoja kwamba Rajoelina lazima achukue hatua za kurejesha imani inayowezesha mazungumzo na kufanya marekebisho ya sheria kabla ya uchaguzi ujao.

Rajoelina alichukua kiti cha rais kwa mara ya kwanza, bila uchaguzi, mwaka 2009 baada ya Ravalomanana kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi.

Rajoelina amesema atatoa kipaumbele kwa suala la uchumi katika muhula wake mpya ili kuimarisha maisha katika nchi hiyo ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, licha ya utajiri wake wa maliasili.

Nchi hiyo ya kisiwa yenye rasilimali nyingi ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa vanila duniani lakini kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo huku kukiwa na mahitaji duni katika miaka ya hivi karibuni kumeathiri sekta hiyo na bajeti ya Madagascar.

Takriban asilimia 75 ya wakazi milioni 29 wa nchi hiyo wanaishi chini ya kiwango cha umaskini.

Baadhi ya wanaharakati wa upinzani wanakabiliwa na mashtaka ya jinai kwa kushiriki maandamano kabla ya uchaguzi ambayo mara nyingi yalivunjwa kwa mabomu ya machozi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live