Rais wa Liberia na mchezaji nyota wa zamani wa soka ya kimataifa George Weah Jumatatu ametangaza kwamba atawania muhula wa pili kwenye uchaguzi wa mwezi Oktoba.
Weah amesema katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa “ Wanainchi wenzangu, nitakuja kwenu hivi karibuni kuwaomba mniongeze tena muhula kwa mara ya pili mlionipa miaka sita iliyopita.”
Weah ameahidi kuwa utakuwa “muhula wa fursa, muhula wa mabadiliko, muhula wa maendeleo”.
Ametetea pia muhula wake wa kwanza, akisema “Nataka niwahakikishie kuwa hali ya taifa letu ni imara. Hali ya taifa letu ni thabiti. Hali ya taifa letu ni ya amani na usalama. Tunakusudia kufanya iendelee hivi.”
Uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 10 Oktoba katika taifa hilo la Afrika magharibi, ambalo bado linaendelea kupata afueni kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mfululizo kati ya mwaka wa 1989 na 2003 ambavyo vilisababisha vifo vya watu 250,000.
Nchi hiyo ilikumbwa na janga la Ebola na taifa hilo lenye watu milioni 5, moja ya nchi maskini duniani, iliathiriwa vibaya na madhara ya uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Nusu ya wanainchi wa Liberia, wanaishi kwa chini ya dola 1.90 kwa siku, kulingana na takwimu za Benki ya dunia.