Kiongozi wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema Mbasogo ametangazwa mshindi wa kiti cha urais kwa muhula wa sita.
Kiongozi huyo ameshinda kwa asilimia 94.9 ya kura zote zilizopigwa. Hayo yameelezwa na maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo mnamo siku ya Jumamosi. Wamesema idadi ya wapigakura ilikuwa asilimia 98 ya raia wote walioandikishwa.
Obiang, mwenye umri wa miaka 80, aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya jeshi ya mnamo mwaka 1979. Hivi sasa Nguema ndiye kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi ukiondoa orodha ya watawala wa kifalme. T
Tangu alipochukua hatamu za uongozi hajawahi kushinda uchaguzi kwa chini ya asilimia 93 ya kura.
Mkuu wa tume ya uchaguzi athibitisha ushindi wa Nguema
Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Guinea ya Ikweta Faustino Ndong Esono Eyang alithibitisha kuwa Obiang ataendelea na wadhifa wa urais kwa muhula mwingine wa miaka saba.
Ushindi huo wa kishindo kwa sehemu kubwa ulitarajiwa kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na linaoongozwa kwa mkono wa chuma.
Mtoto wa kiume wa rais Teodoro Obiang Nguema ni makamu wa rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Nguema Obiang Mangue. Kwa jumla upinzani wa taifa hilo ni dhaifu na chama cha Obiang cha Democratic Party of Equatorial Guinea (PDGE) kina nguvu kubwa.
Katika uchaguzi wa mwaka huu uliofanyika Jumapili iliyopita, Nguema alikuwa akiungwa mkono na muungano wa vyama vya siasa 15 ikiwemo chama chake cha PDGE.
Chama hicho ambacho ndiyo kilikuwa taasisi halali ya kisiasa nchini Guinea ya Ikweta hadi mwaka 1991, kimeshinda pia viti vyote vya Bunge la Taifa na Baraza la Seneti.
Hata hivyo tume ya uchaguzi haikutangaza asilimia ya matokeo waliyopata wagombea wa urais wa upande wa upinzani ambao ni Andres Esono Ondo wa chama cha Convergence for Social Democracy na Buenaventura Monsuy Asumu wa chama cha Social Democratic Coalition Party.
"Kwa mara nyingine matokeo ya mwisho ya uchaguzi yameonesha kuwa upande wetu" aliandika kupitia ukurasa wa Twitter mtoto wa kiume wa rais Obiang, ambaye ni makamu wa rais wa nchi hiyo Teodoro Nguema Obiang Mangue.
Ujumbe wake uliongeza kwamba "tutaendelea kuthibitisha kwamba sisi ni chama kikubwa.." Obiang, mtawala wa mkono wa chuma anayeshutumiwa kwa ufisadi na ukandamizaji upinzani
Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta
Obiang ameitawala Guinea ya Ikweta kwa zaidi ya miaka 43 baada ya kumpindua mjomba wake, Francisco Macias Nguema, ambaye baadae alihukumiwa kuuwawa kwa kupigwa risasi.
Tangu alipoingia madarakani amekuwa akikandamiza kila aina ya upinzani na ukosoaji na amefanikiwa kuzuia majaribio kadhaa ya mapinduzi kwenye taifa hilo ambalo ni koloni la zamani la Uhispania.
Kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi vikosi vya usalama viliwakamata wanasiasa kadhaa wa upinzani chini ya kile utawala wa nchi hiyo ulikitaja kuwa kuzima "njama" za kufanyika mashambulizi kwenye mji mkuu Malabo na katika mji mkubwa wa kibiashara wa Bata.
Serikali pia iliifunga mipaka yake ya ardhini na mataifa jirani ya Gabon na Cameroon kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi, ikisema inazuia wahujumu kutovuruga uchaguzi.
Obiang ni rais wa pili wa Guinea ya Ikweta tangu taifa hilo lipopopata uhuru mwaka 1968 kutoka Uhispania, iliyokuwa mtawala wake wa kikoloni kwa karibu karne mbili. Licha ya utajiri mkubwa wa mafuta, taifa analoongoza linaorodheshwa kuwa miongoni mwa yale masikini zaidi duniani.
Rushwa na ufujaji wa mali ya umma ni masuala yanayotajwa kukita mizizi ndani ya utawala wa miongo minne wa familia ya Nguema.