Watu 11 waliotuhumiwa kula njama ya kufanya mapinduzi nchini Chad wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, lakini mwanasheria mkuu mjini N’Djamena amevieleza vyombo vya habari kuwa ofisi ya rais imesema wahukumiwa hao watasamehewa.
Mapema mwezi Januari, serikali ya Chad ilitangaza kuwa maafisa kumi wa jeshi na mwanaharati maarufu wa haki za binadamu Berdei Targuio walikamatwa wakishtumiwa “kujaribu kuvuruga utaratibu wa kikatiba” na taasisi za nchi.
Berdei Targuio aliyetambulishwa na mamlaka kama kiongozi wa mpango huo wa kufanya mapinduzi mwezi Disemba, ni mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Chad (OTDH) na mkosoaji mkubwa wa utawala.
Watu wao 11, ambao wamezuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Koro Toro, lililoko umbali wa kilomita 600 kaskazini mwa mji mkuu N’Djamena, walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuvunja utaratibu wa kikatiba, kumiliki silaha kinyume cha sheria na kushirikiana na wahalifu. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la taifa.