Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby ametangaza msahama kwa mamia ya waasi waliohukumiwa kifungo cha maisha jela hivi karibuni, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya rais wa zamani wa Mali Idriss Deby Itno, ambaye ni baba ya rais huyo wa muda.
Waasi hao 380 ni miongoni mwa wanachama 400 wa kundi la waasi la Front for Change and Concord in Chad (FACT) ambao mahakama nchini Chad Jumanne iliyopita ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi yao.
Wanatuhumiwa kuhusika katika kumuua rais wa zamani Idriss Deby, ambaye aliuawa akiwa katika medani ya vita dhidi ya kundi hilo la waasi mnamo mwaka 2021.
Hata hivyo kiongozi wa kundi hilo la waasi, Mahamat Ali Mahadi, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela bila ya kuwepo mahakamani, hajajumuishwa kwenye msamaha huo wa rais.
Kesi ya wanachama 465 wa kundi la waasi la FACT lenye makao yake nchini Libya ilianza Februari 13 katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena. Mahakama iliwapata na hatia ya vitendo vya ugaidi waasi 441 ambapo walikabiliwa na mashtaka kadhaa.
Msemaji wa FACT, Adoum Chouwimi amesema kesi hiyo ilikuwa na dosari na kuutaja uamuzi huo kuwa uongo mtupu.
Deby, aliyekuwa na umri wa miaka 68 alipigwa risasi alipowatembelea wanajeshi waliokuwa kwenye mstari wa mbele dhidi ya waasi wa FACT ambao walikuwa wamesogea kusini kutoka mpaka wa kaskazini mwa Chad na Libya, na walikuwa wanasonga mbele kuelekea mji mkuu.
Taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati linalotawaliwa na jeshi limekuwa katika mgogoro tangu kifo cha Rais Idriss Deby Itno mnamo Aprili 2021, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.