Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais auawa na waasi, mwanawe akabidhiwa nchi

290bc43b9bc1f68d0c352f4598665878 Rais auawa na waasi, mwanawe akabidhiwa nchi

Wed, 21 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Chad limetangaza kuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby (69) amefariki dunia baada ya kupata majeraha kwenye mapambano dhidi ya waasi.

Mwishoni mwa wiki Deby alienda kuvitembelea vikosi vya nchi hiyo vilivyopo kaskazini vinavyopambana na waasi wanaodaiwa kutokea Libya.

Kifo chake kimetokea ikiwa ni saa chache tu tangu matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Aprili 11 kuonesha kuwa anaongoza kwa asilimia 80.

Kwa ushindi huo, Deby angeiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita mfululizo.

Serikali na Bunge vimevunjwa na sasa baraza la kijeshi ndilo litakaloiongoza nchi hiyo kwa miezi 18 ijayo.

Deby aliingia madarakani mwaka 1990 baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Waasi kutoka kundi linalojiita Fact (the Front for Change and Concord in Chad), walishambulia kituo cha mpaka wa Libya na Chad siku ya uchaguzi, Aprili 11 na walikuwa wakienda mji mkuu wa N’Djamena.

Mapambano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yalianza Jumamosi.

Jenerali wa jeshi alisema kuwa waasi 300 waliuawa na wengine 150 walikamatwa katika mapambano hayo.

Aliongeza kuwa jeshi lilipoteza askari watano na wengine 36 walijeruhiwa.

Hata hivyo idadi hiyo haikuthibitishwa. Deby kwa muda mrefu amekuwa mshirika mkubwa wa Ufaransa na mataifa mengine ya Magharibi.

Hata hivyo kumekuwa na ongezeko la ukosoaji ndani ya nchi kwa namna ambavyo serikali yake ilikuwa ikitumia mapato yatokanayo na mauzo ya mafuta.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, aliahidi kurejesha amani na ulinzi katika ukanda huo.

Msemaji wa jeshi alinukuliwa akisema kuwa mtoto wa rais aliyeuawa ndiye atakayeliongoza baraza la kijeshi linaloiongoza nchi hiyo. Mtoto huyo, Mahamat Idriss Deby ni mwanajeshi wa cheo cha juu cha jenerali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz