Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amewataka Wamisri kuwa na watoto wachache, akisema kwamba kiwango cha sasa cha kuzaliana kitaleta "janga" kwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.
"Tunahitaji watoto 400,000 wanaozaliwa kwa mwaka," al-Sisi aliliambia Kongamano la Kimataifa la Idadi ya Watu, Afya na Maendeleo (Global Congress on Population, Health and Development (PHDC)), ambalo lilifunguliwa mjini Cairo siku ya Jumanne.
"Sikubaliani na wazo kwamba kuwa na watoto ni suala la uhuru kamili," rais alisema. "Kuacha uhuru wao kwa watu ambao labda hawajui ukubwa wa changamoto? Mwishowe, ni jamii nzima na taifa la Misri ambalo litalipa gharama hiyo,” al-Sisi alisema. "Lazima tupange uhuru huu, vinginevyo utaleta janga."
Alitoa mfano wa China, ambayo "ilifanikiwa kudhibiti idadi ya watu" kwa kuweka sera kali ya mtoto mmoja katika miaka ya 1970. Beijing iliachana na sera hiyo mwaka 2015, lakini tangu wakati huo imehimiza ongezeko la watu.
Kulingana na mkutano wa PHDC, ukuaji wa idadi ya watu unaweza "kuweka mzigo kwenye rasilimali na miundombinu, na kusababisha changamoto za kiafya na kijamii." Idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi "inahatarisha upatikanaji na ubora wa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na, afya, elimu, hifadhi ya jamii" na kuchangia "kupungua kwa kasi kwa maliasili," nyaraka zilisema.
Mkutano huo, ulioanza Jumanne na umepangwa kuendelea hadi Septemba 8, unafadhiliwa na mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa, USAID, na makampuni kadhaa makubwa ya dawa.