Duru zimeeleza kuwa baadhi ya mawaziri katika serikali ya Rais William Ruto wametamaushwa na hali ya kudorora kwa uchumi wa nchi, ambapo sasa wamepanga kujiuzulu.
Ripoti zimeeleza baadhi yao hata wamewasilisha barua za kujiuzulu kwa Rais, ingawa amezikataa.
Kulingana na duru hizo, mwishoni mwa mwaka uliopita, Rais Ruto aliripotiwa kukataa barua ya kujiuzulu ya Waziri wa Fedha, Profesa Njuguna Ndung’u.
“Kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita, Waziri [Ndung’u] aliwasilisha barua ya kujiuzulu. Inaripotiwa kwamba amesikitishwa na mkondo ambao nchi imechukua na hataki kuchukua lawama,” zikaeleza duru.
Duru zilieleza kuwa baadhi ya malalamishi yaliyopo ni [Waziri] kutojumuishwa kwenye masuala muhimu, kama vile maamuzi kuhusu ushuru.
“Waziri anahisi kutengwa kwenye masuala muhimu yanayohusu uendeshaji wa uchumi wa nchi. Anaogopa kuwa huenda akaelekezewa lawama kwa sera au hatua ambazo hakuhusika kuzitekeleza,” zikaeleza duru.
Kwa muda wa mwaka mmoja uliopita, serikali ya Rais Ruto imejipata lawamani kutokana na hatua yake ya kuendelea kuongeza ushuru, hasa miongoni mwa wafanyakazi wenye ajira rasmi.
Baadhi ya ushuru ambao imeanza kutekeleza ni makato ya nyumba, kuongeza makato ya Hazina ya Kitaifa ya Uzeeni (NSSF) na makato ya Bima ya Kitaifa, SHIF kwa asilimia 2.75.
Wadadisi wa masuala ya kiuchumi wamekuwa wakisema kuwa hatua nyingi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na serikali zinatokana na masharti ambayo imekuwa ikipewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Kufikia sasa, Kenya imechukua jumla ya Sh704 bilioni kutoka kwa shirika hilo, baada ya serikali kupewa mkopo wa Sh150 bilioni zaidi mnamo Jumatano, Januari 17, 2024.