Rais wa Zimbabwe, kiongozi mkuu wa upinzani pamoja na kiongozi wa zamani wa chama tawala aliyekuwa uhamishoni kufuatia mapinduzi ni miongoni mwa watakaowania urais, katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Agosti.
Viongozi hao watatu tayari wamesajiliwa kugombea nafasi hiyo na tume ya taifa ya uchaguzi, ambayo inatarajia kutangaza orodha ya mwisho ya wagombea waliothibitishwa.
Rais Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF anawania awamu ya mwisho na anatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa, aliyemshinda kwa umbali mdogo katika uchaguzi uliotawaliwa na mzozo wa mwaka 2018.
Aliyewahi kuwa waziri kwenye serikali ya Robert Mugabe, Saviour Kasukuwere, aliyekimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini baada ya mapinduzi ya mwaka 2017, pia anawania nafasi hiyo, ingawa bado haijulikani kama tayari amerejea nchini humo.
Uchaguzi huu wa Agosti unatarajiwa pia kufuatiliwa kwa karibu, katika taifa hilo lenye historia ya uchaguzi unaogubikwa na machafuko na mivutano.
Wakati huo huo, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameonya dhidi ya sauti za kigeni au za ndani, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyo ya uaminifu ambayo yanachochea migawanyiko na mifarakano.
Emmerson Mnangagwa ambaye ameshindwa kuboresha hali ya uchumi iliyodorora kwa miaka ishirini sasa licha ya ahadi alizotoa, analaumiwa na wananchi kwa hali ngumu iliyonayo Zimbabwe.