Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Weah mambo magumu uchaguzi wa marudio Liberia

Rais Liberia; George Weah Rais Weah mambo magumu uchaguzi wa marudio Liberia

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamke akipiga kura yake katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Liberia mjini Monrovia, Jumanne, Novemba 14, 2023.

Nyota huyo wa zamani wa soka wa kimataifa huenda alimshinda kwa urahisi Joseph Boakai katika duru ya pili ya 2017, lakini matokeo ya duru ya kwanza ya kura mwezi uliopita yanaonyesha kukaribiana sana: Weah alipata asilimia 43.83 huku Boakai akijikinfia asilimia 43.44 ya kura jumla.

"Tunaenda kwenye uchaguzi ambapo hakuna mtu ana uwezo wa ushindani na tofauti kubwa," alisema Ibrahim Nyei, mkurugenzi mtendaji katika Taasisi ya Ducor ya Utafiti wa Kijamii na Kiuchumi.

Katika wiki kadhaa tangu duru ya kwanza ya Oktoba 10, wagombea wote wawili wamekuwa wakitafuta ridhaa kutoka kwa vyama vingine vidogo vya upinzani. Kufikia sasa, Boakai amefanikiwa kuungwa mkono na washindi wa tatu, wa nne na wa tano.

Ingawa hiyo ni sawa na asilimia 5.6 tu ya kura, inaweza kuelekeza kura upande wa Boakai. Wakati huo huo, Weah amepata kuungwa mkono na vyama vingine viwili vya upinzani.

Raia wa Liberia wanaweza kusubiri matokeo kwa muda mrefu: Iliwachukua maafisa wa uchaguzi wiki mbili kutangaza matokeo ya duru ya kwanza na haja ya kufanyika kwa duru ya marudio. Katika hotuba ya mwisho kwa wapiga kura, Weah alisisitiza kuwa "uchaguzi huu wa marudio sio tu wa kunichagua tena kama rais kwa muhula wa pili."

"Unahusu mustakabali wa Libeŕia. Unahusu watoto wenu, familia zenu, jumuiya zenu, na vizazi vijavyo,” Weah alisema. "Kwa pamoja, tutaendelea kutengeneza njia kuelekea maendeleo, amani na ustawi."

Ushindani mkali Weah alishinda uchaguzi wa 2017 huku kukiwa na matumaini makubwa yaliyoletwa na ahadi yake ya kupambana na umaskini na kukuza maendeleo ya miundombinu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kukabidhiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mfululizo kati ya 1989 na 2003 ambavyo viliua takriban watu 250,000.

Lakini rais huyo mwenye umri wa miaka 57 ameshutumiwa kwa kutotimiza ahadi muhimu za kampeni kwamba angepambana na ufisadi na kuhakikisha haki kwa wahanga wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Boakai, 78, amefanya kampeni kwa ahadi ya kuinusuru Liberia kutokana na kile alichokiita uongozi uliofeli wa Weah. Hapo awali aliwahi kuwa makamu wa rais wa Liberia chini ya Ellen Johnson Sirleaf, kiongozi mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia.

"Uchaguzi huu wa marudio unawakilisha msukumo wa mwisho wa kuondoa ugaidi, uvunjaji wa sheria, ufisadi, kutojali, kupuuzwa na uzembe ambao umeikumba nchi yetu kwa miaka sita," aliwaambia Waliberia katika hotuba yake ya mwisho kabla ya kura ya Jumanne.

"Tuna imani kwamba Waliberia watajitokeza tena kwa wingi wao ili kuonyesha upendo wao, ujasiri, uthabiti, na azma ya kuungana nasi katika kuikomboa nchi yetu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live