Wakili msomi nchini Kenya aliyefurushwa nchini humo Miguna Miguna ana furaha isiyokuwa na kifani baada ya kukabidhiwa pasipoti mpya ya Kenya anapotazamia kurejea nyumbani ambapo amesema kuwa Rais William Ruto ndiye alimsaidia kupata pasipoti mpya
Miguna alisema sasa anasubiri tu vikwazo vilivyowekwa dhidi yake kuondolewa ili kumruhusu kurejea nyumbani.
"Rais William Samoei Ruto ameniletea pasipoti mpya. Sikuhitajika kutia sahihi fomu za kipuuzi walizokuwa wakizungumzia. Nasubiri kuondolewa kwa vikwazo," alisema.
Miguna alisema vikwazo hivyo ambavyo ni vizingiti kwake kurejea nyumbani, vitaondolewa Jumatano, Septemba 14.
"Ninafuraha kutangaza kwamba Rais @WilliamsRuto amenihakikishia kwamba vikwazo vitaondolewa Jumatano, Septemba 14, 2022. Baadaye, nitaundiwa upya Pasipoti yangu ya Kenya, na nitatangaza tarehe ya kurudi kwangu nyumbani. Bravo!" aliandika.
Miguna alikuwa na matumaini ya kurejea Kenya baada ya Ruto kutangazwa Rais mteule. Miaka minne baada ya kufukuzwa nchini na kurejeshwa Canada, Miguna Miguna alikuwa na imani ya kurejea nyumbani lakini juhudi zake ziliambulia patupu baada ya kuzuiwa mwaka wa 2020.
Kwa muda wa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi, Miguna amekuwa akimpigia debe Ruto, akimsifu namna utawala wake ungeng'oa enzi ya matajiri waliotawala siasa za Kenya kwa miaka mingi.
"Kwa wazalendo wote: Tulieni. Asante kwa mshikamano. Ndiyo, nimepakia virago vyangu, na niko tayari. Lakini kabla sijaweza kurejea nyumbani, William Samoei Ruto lazima aapishwe kwanza, vikwazo viondolewe, na pasipoti yangu ya Kenya kufanywa upya. Tutaonana hivi karibuni. Cheers!," alisema Miguna.