Rais wa Kenya, William Ruto amesema maandamano ya amani ya Generation Z yaliingiliwa na wahalifu, akisisitiza Serikali itazingatia mamlaka yake ya kikatiba ya kulinda Taifa kutokana na vitendo hivyo.
Amesema tukio la vurugu katika maandamano ya jana Juni 25, 2024 linatoa somo la namna ya kukabiliana na vitisho vya usalama wa Taifa.
“Ninawahakikishia Wakenya kwamba, Serikali imekusanya rasilimali zote kuhakikisha hali ya namna hii haitajirudia kwa gharama yoyote ile,” amesema Rais Ruto.
Amewashukuru maofisa wa ulinzi kwa kazi kubwa waliyoifanya kukabiliana na ghasia za maandamano hayo katika harakati za kuilinda Kenya na watu wake.
“Nimeviagiza vyombo vyote vya usalama wa Taifa kuweka mikakati kuzuia jaribio lolote la wahalifu hatari wanaotaka kuvunja usalama na utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Akihutubia Taifa mubashara amewahakikishia Wakenya usalama wao ndiyo kipaumbele chake.
Pia, amewashukuru vijana wa Kenya waliojitoa kufanya mazungumzo yasiyo na misingi ya kikabila, bali katika masuala ya kisera, akisema matokeo yake yanaonekana.
“Majadiliano ya kitaifa lazima yafanyike katika namna ambayo inaheshimu misingi ambayo nchi yetu imejengwa kama vile ukuu wa Katiba, utawala wa sheria na kuheshimu taasisi.
“Inaumiza kwamba mazungumzo haya muhimu yalivamiwa na watu hatari ambao wametusababishia hasara kama Taifa leo. Inawezekana wahalifu hawa waliojitokeza kutikisa usalama wetu, wakajaribu tena,” amesema.
Ameahidi usalama kwa wananchi dhidi ya wanaopanga, wanaofadhili, na watekelezaji wa ghasia zinazotokea nchini Kenya, lengo likiwa ni kuhakikisha Taifa hilo linaendelea kuwa salama.
Rais Ruto amesisitiza kuendelea kusimamia misingi ya Katiba, akisema nguvu ya Serikali itatoka kwa wananchi, lakini kwa kuhakikisha jambo hilo linafuata njia za kikatiba.
Awali, Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Aden Duale alitangaza askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusambazwa kutokana na mfululizo wa maandamano yanayolenga kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024.
Katika gazeti la Serikali la Juni 25, 2024, Waziri wa Ulinzi alitumia kifungu cha 241 (3) (b) cha Katiba ya Kenya kutangaza kutumwa Jeshi la Ulinzi la Kenya kulisaidia Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa Duale, kutumwa kwa wanajeshi wa KDF kumetokana na maandamano ya ghasia yanayoendelea maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kenya, ambayo yamesababisha uharibifu na uvunjifu wa miundo muhimu.
“Vikosi vya Ulinzi vya Kenya vitatumwa Juni 25, 2024 ili kusaidia Huduma ya Kitaifa ya Polisi katika kukabiliana na dharura ya usalama iliyosababishwa na maandamano ya ghasia yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kenya na kusababisha uharibifu na uvamizi wa miundombinu muhimu,” tangazo katika gazeti la Serikali linasomeka.
Wakati huohuo, Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika taarifa ameeleza kusikitishwa na vifo vilivyotokea kutokana na kinachoendelea nchini humo, akieleza ni haki ya wananchi kuandamana na pia ni wajibu wa viongozi kusikiliza.
“Katika kipindi hiki cha majaribu, ninawakumbusha viongozi wote kwamba walichaguliwa na watu. Kuwasikiliza watu siyo chaguo, bali ni lazima kama ilivyoainishwa kwenye misingi ya Katiba na kama ilivyo msingi wa falsafa ya demokrasia,” amesema Kenyatta.
Amesisitiza viongozi watambue wanapata nguvu na mamlaka kutoka kwa wananchi.
“Wapendwa Wakenya, nasimama nanyi na ninaomba viongozi wetu watumie mazungumzo, na kuzungumza na watu. Ninaomba amani na maelewano kwa kila Mkenya na kwetu sote kukumbuka kwamba, Kenya ni kubwa kuliko mtu mmoja,” amesema Kenyatta.