Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesitisha mpango wake wa kuhudhuria Kongamano la Kiuchumi Duniani (WEF) mjini Davos kwasababu ya tatizo la nishati linaloendelea nchini mwake, msemaji wake amesema.
Taifa hilo linakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la umeme kuwahi kutokea huku watu wakikabiliwa na kukatika kwa umeme hadi saa sita kwa siku.
Bw Ramaphosa alipaswa kuongoza wajumbe wa serikali yake kwenye kongamano hilo, shirika la habari la AFP linaripoti.
Lakini badala yake atafanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa na kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali ya Eskom, alisema msemaji wa rais Vincent Magwenya.
"Rais Cyril Ramaphosa tayari amezungumza na uongozi wa Eskom na kamati ya Kitaifa ya kutatua changamoto za Nishati (NECCOM) na mikutano hiyo itaendelea," alisema.