Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Nyusi: Magufuli alijali maslahi ya Watanzania

870e3919fb75d0f3f68584531be48104.jpeg Rais Nyusi: Magufuli alijali maslahi ya Watanzania

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais wa Msumbuji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Filipe Nyusi amesema Rais Magufuli alitetea maslahi bora na makuu ya raia wa Tanzania.

Aidha amesema hatua za Rais Magufuli na kuhusika kwake kama kiongozi, zimemfanya kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa na historia ya hivi karibuni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kusini mwa Afrika, Afrika ya Mashariki, na Bara za la Afrika.

Rais Nyusi amebainisha kuwa eneo la Kusini mwa Afrika limepoteza mmoja wa wanaye mashuhuri. Pia ameweka wazi kuwa watanzania wamempoteza raia mwaminifu, mtanzania mfanyaji kazi na mwenye imani za kipekee, ambazo zimekuza Taifa la Tanzania na bara lote la Afrika.

Mbali na hayo, amebainisha kuwa Rais Magufuli aliongoza SADC kwa kujitolea, na kuwa alikuwa na tamaa ya kuiona Kanda ya Kusini mwa Afrika ikiwa huru kutoka katika utegemezi wa kiuchumi.

Rais Nyusi ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Magufuli Tanzania na Afrika kuwa ni pamoja na utulivu wa kisiasa wenye sifa nzuri na za wazi, ustawi wa kijamii na kiuchumi wa Tanzania, miundombinu ya msingi kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha ya watanzania, viwango vya juu vya ufanisi na utendaji bora vya serikali.

Akitoa sababu ya kutoa hotuba yake kwa Lugha ya Kiswahili, Rais Nyusi amebainisha kuwa hiyo ni sehemu ya kuheshimu kauli ya Magufuli alipotangaza Kiswahili kuwa Lugha ya SADC, katika mojawapo ya mikutano ya jumuiya hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz