Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Nkurunziza ajiandalia mabilioni ya kustaafu

92899 Pic+nkurunzinza Rais Nkurunziza ajiandalia mabilioni ya kustaafu

Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bunge la Burundi limepitisha sheria itakayompa rais mstaafu mafao ya faranga bilioni moja (zaidi ya Sh1 bilioni za Tanzania), kiwango ambacho kinatajwa ni kikubwa ukilinganisha na nchi nyingine Afrika Mashariki.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni miezi minne tangu Rais wa sasa wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kutamka kuwa hatagombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa Mei 20, mwaka huu.

Wabunge walipitisha sheria hiyo kwa kura 98 huku wawili pekee wa upinzani wakiipinga.

Wakati wa mjadala, wabunge walipendekeza kiwango atakachopewa rais anayeondoka madarakani, huku baadhi wakisema apewe faranga milioni 500, wengine wakisema apewe faranga bilioni moja na wengine wakisema apewe faranga bilioni mbili, wakapitisha faranga bilioni moja na marupurupu.

Vilevile, wabunge hao walipendekeza Nkurunziza apewe cheo cha ‘Kiongozi Mkuu na Bingwa wa Uzalendo’.

Pendekezo hilo lilipitishwa baadaye na Baraza la Mawaziri katika jimbo la kisiasa la Gitega nchini Burundi, kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter wa msemaji wa Rais wa Burundi.

Pia Soma

Advertisement
Mbali na kitita cha mkupuo, sheria hiyo inataka Rais mstaafu aendelee kupewa stahiki sawa na makamu wa rais aliye madarakani kwa kipindi cha miaka saba, na baada ya hapo atapewa stahiki sawa na mbunge.

Kiwango hicho kinaelezwa ni kikubwa kulinganisha na uchumi wa Burundi, nchi ambayo asilimia 65 ya watu wake ni masikini na karibu nusu ya nchi ina upungufu wa chakula, kwa mujibu wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Kiongozi wa upinzani nchini Burundi, Agathon Rwasa alisema fedha hizo ni nyingi mno kutolewa na Serikali hasa ukizingatia uchumi wa nchi hiyo bado haujatengemaa.

Mafao zaidi

Akifafanua kuhusu sheria hiyo bungeni jana, waziri wa sheria, Aimé Laurentine Kanyana alisema rais atakapostaafu atachukuliwa kwa hadhi ya makamu wa rais kwa kipindi cha miaka saba.

“Chini ya utaratibu huo atakuwa na haki ya kupatiwa magari sita na madereva saba lakini pia yeye na familia yake watapewa hati ya kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia.

“Baada ya miaka saba, rais mstaafu atachukuliwa kama mwenye cheo cha ubunge,” alisisitiza Waziri Kanyana.

Sheria hiyo inasema “Rais mstaafu atajengewa ‘jumba la kifahari’ kwa fedha za umma katika eneo atakalochagua yeye ndani ya miaka mitano.

Gharama za jumba litakalojengwa hazijawekwa bayana.

Kwa mujibu wa Waziri Kanyana, sheria hiyo itamhusu rais aliyepo sasa na watangulizi wake ambao waliingia madarakani bila mapinduzi ya kijeshi.

Hivyo, ni Rais Melchior Ndadaye, aliyeuawa mwaka 1993 na Nkurunziza pekee wenye vigezo vya kupewa marupurupu hayo.

Kauli ya upinzani

Agathon Rwasa, Spika wa Bunge alisema huenda chama tawala chenye wingi wa wabunge kilikusudia kumpa maisha mazuri Rais Nkurunziza baada ya kustaafu ili asiwe na nia ya kugombea tena.

Hata hivyo, Rwasa aliongeza kuwa usalama wa nchi ni muhimu kuliko marupurupu.

Wakati upinzani wakiona hivyo, Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kwa jicho moja unaweza kusema ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa Burundi ni nchi maskini inayohitaji fedha nyingi za miradi ya maendeleo.

“Lakini kwa upande mwingine wa kisiasa, huenda Bunge limetafutia Nkurunziza namna nzuri ya kuondoka madarakani. Ni njia salama ambayo yeye ataendelea kujiona ana mamlaka makubwa hata baada ya kustaafu,” alisema Dk Mbunda.

Kuachia madaraka 2020

Juni 2018, Rais Nkurunziza alidokeza kwa mara ya kwanza kwamba hataomba tena baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2020.

Alitoa tangazo hilo akiwa eneo la Bugendana, Gitega ambapo alikuwa anazindua katiba mpya ya nchi hiyo, ambayo hata hivyo ilikuwa inampa fursa ya kuendelea.

Alizindua katiba hiyo iliyopitishwa na raia wa nchi hiyo kwa wingi na kubadilisha muhula wa rais kutoka miaka mitano kuwa saba.

Wengi waliamini kuwa Nkurunziza ndiye aliyeshinikiza kufanyika kwa mabadiliko hayo ili kumpa fursa ya kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura hiyo, waliounga mkono marekebisho hayo walikuwa asilimia 73.6, waliopinga walikuwa asilimia 19.3 na kura asilimia 4.1 ziliharibika. Asilimia 3.2 hawakuunga mkono upande wowote.

Kwa marekebisho hayo, Nkurunziza angeweza kuwania tena urais mwaka 2020, mihula mingine miwili ambayo ingeanza kuhesabiwa chini ya katiba mpya.

Mafao nchi jirani

Pamoja na utofauti wa kiwango cha mafao, suala la Nkurunziza si la kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko duniani.

Nchini Tanzania, kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1999, ambayo ilirekebishwa mwaka 2005, Rais mstaafu anapomaliza kipindi chake cha uongozi, hupata mafao ya mkupuo ambayo hukokotolewa kwa kuzingatia mshahara wa juu aliowahi kupata, pamoja na kiwango cha asilimia itakayopangwa na mamlaka husika.

Mbali ya mafao hayo ambayo hayako bayana, Rais mstaafu hulipwa posho ya kila mwezi sawa na asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani.

Rais pia hupewa ulinzi yeye na familia yake, msaidizi, katibu muhtasi, mhudumu wa ofisi, mpishi, dobi, mtumishi wa ndani, mtunza bustani, madereva wawili na gharama za mazishi atakapofariki.

Vilevile Rais hupewa pasi ya kusafiria yenye hadhi ya kidiplomasia, yeye pamoja na mke au mumewe na pia wote wawili hugharamiwa matibabu ndani au nje ya nchi.

Kiongozi huyo mstaafu pia hulipiwa matengenezo ya magari mawili yenye uzito usiopungua tani tatu, ambayo hutolewa na Serikali, na ambayo pia hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Zaidi ya hapo, Rais mstaafu hujengewa nyumba mpya, ambayo ni lazima iwe na vyumba angalau vinne, viwili kati ya hivyo viwe na huduma zote ndani (self-contained). Nyumba hiyo ni lazima iwe na ofisi iliyokamilika na nyumba kwa ajili ya mfanyakazi.

Mafao ya Rais mstaafu Kenya

Hata kwa Kenya hali zi tofauti, kwani Rais mstaafu amewekewa mazingira mazuri ya kustaafu.

Siku chache kabla hajaondoka madarakani, Rais Mwai Kibaki alisaini sheria iliyoweka kiwango cha Shilingi za Kenya 16.8 milioni (378 milioni za Tanzania) kama mafao ya mkupuo, pensheni ya KSh560,000 (Sh12.6 milioni za Tanzania kila mwezi) na posho nyingine zinazofikia Ksh13 milioni (Sh292 milioni za (Tanzania) kwa mwaka.

Sheria hiyo ilikuwa inarekebisha ile ya mwaka 2002 iliyokuwa inabainisha kuwa mafao ya mkupuo ya Rais ni sawa na jumla ya mishahara yake ya mwaka mmoja aliohudumu kwa kila muhula.

Sheria hiyo pia ilikuwa inainisha viwango vya magari, watumishi, wasaidizi na posho za nyumba.

Chanzo: mwananchi.co.tz