Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Mpya wa Sri Lanka atoa tamko zito baada ya kuapishwa

Rais Mpya Wa Sri Lanka Rais Mpya wa Sri Lanka atoa tamko zito baada ya kuapishwa

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Siku moja baada ya kula kiapo cha kuongoza Sri Lanka kwa mpito, Ranil Wickremesinghe ametoa angalizo kwa makundi yanayotumia maandamano nchini humo kufanya uharibifu, huku akiahidi kurejesha misingi ya amani kwa wananchi wa Taifa hilo waliokuwa mjadala na gumzo duniani.

Wananchi hao waligeuka habari na mjadala mkubwa kila kona duniani, hususan mitandao ya kijamii, baada ya kuandamana kabla ya kulizidi nguvu jeshi la nchi hiyo na kuingia ikulu ya Rais Gotabaya Rajapaksa kisha kufanya uharibifu wa vifaa na kujivinjari watakavyo.

Maandamano hayo yanafanyika kwa zaidi ya wiki mbili sasa na kusababisha watu 42, wakiwemo wanajeshi wawili kujeruhiwa.

Mbali ya hilo, maandamano hayo pia yalisababisha aliyekuwa Rais, Gotabaya Rajapaksa kuikimbia nchi hiyo. Rajapaksa, mkewe na walinzi wawili waliwasili mji wa Singapore wakitokea visiwa vya Maldives alikokimbilia Jumatano iliyopita.

Baada ya tukio hilo, Alhamisi Spika wa Bunge, Mahinda Yapa Abeywardena alipokea barua rasmi ya kujiuzulu kwa Rajapaksa, iliyowasilishwa kwake kupitia ofisi ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Singapore.

Ijumaa wabunge wa Bunge la nchi hiyo walikutana kujadili na kufanikisha mchakato wa kumpata Wickremesinghe.

Advertisement Wickremesinghe ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Taifa hilo, aliapishwa juzi kwa ajili ya kurejesha amani na utawala wa kisheria kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais kuziba nafasi ya Rajapaksa.

Baada ya kuingia Ikulu, Wickremesinghe alihutubia taifa akisema anakubali haki ya watu kufanya maandamano ya amani, huku akilaani baadhi wanaotumia maandamano hayo kufanya vurugu na kushambulia vikosi vya usalama.

Awali kabla ya Wickremesinghe kukabidhiwa majukumu hayo, Spika wa Bunge alisema mchakato wa kumteua Rais mpya utachukua siku saba, huku akifafanua mamlaka ya Wickremesinghe kumteua waziri mkuu mpya, ambaye pia atapitia mchakato wa kuidhinishwa na Bunge.

Katika sehemu ya hotuba yake, Spika Abeywardana aliwaomba wananchi kudumisha amani.

“Nawaomba wananchi wenye upendo kwa nchi hii, kuweka mazingira ya amani ili kuwawezesha wabunge wote kushiriki katika mikutano na kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa uangalifu,” alisema.

Hatua ya wananchi hao kuandamana inachagizwa na nchi hiyo kukosa fedha za kigeni zinazowezesha kulipia uagizaji bidhaa za kimsingi na mahitaji kama vile chakula, mbolea, dawa na mafuta kutoka nje.

Baadhi ya wachumi wamekuwa wakishangazwa na changamoto ya kushuka kasi ya ukuaji uchumi wa taifa hilo, lililokuwa na uchumi imara kabla ya mgogoro huu.

Awali Serikali ya Sri Lanka ilianza majadiliano na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu mkopo utakaowakwamua katika hali hiyo ya kiuchumi, kabla majadiliano hayo kusitishwa baada ya tishio la maandamano dhidi ya serikali.

Msemaji wa IMF, Gerry Rice aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa wafanyakazi wa hazina bado wanawasiliana na maofisa wa Serikali katika ngazi ya kiufundi na wanatarajia kuanza tena mazungumzo mara tu inapowezekana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa katika vyombo vya habari, tayari Sri Lanka imeshapokea msaada wa fedha kutoka India, huku ikiwa katika mazungumzo ya karibu ili kupata msaada mwingine kutoka China.

Katiba imeelekeza nini baada ya Rais kujiuzulu?

Kwa mujibu wa katiba ya Sri Lanka, iwapo Rais atajiuzulu, barua ya kujiuzulu lazima iwasilishwe kwa Spika. Halafu kazi ya urais inakuwa wazi.

Ofisi ya Rais ikiwa wazi, Waziri Mkuu huwa Kaimu Rais. Kama Waziri Mkuu hawezi kufanya hivyo, Spika anaweza kuwa Kaimu Rais.

Sheria inawaruhusu wabunge kumteua Rais katika kipindi cha siku 30 na kwa kawaida huwa anachaguliwa kwa kura ya siri bungeni. Kushinda kura hiyo, atatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Ili kuchaguliwa kuwa Rais, mgombea lazima apate kura 113 kati ya wabunge 225 wa bunge la Sri Lanka.

Chanzo: Mwananchi