Rais mteule wa Liberia Joseph Boakai ataapishwa Jumatatu hii, Januari 22, 2024, mjini Monrovia, kwa muhula wa miaka sita, baada ya ushindi wake mwishoni mwa mwezi wa Novemba dhidi ya nyota wa zamani wa kandanda George Weah.
Bw. Boakai, mwenye umri wa miaka 79, ataapishwa uani kwenye makao makuu ya Baraza la Bunge, mbele ya wajumbe wa kigeni wakiwemo wakuu wa nchi, kulingana na mpango rasmi.
Joseph Boakai ni mkongwe wa siasa za Liberia, akihudumu kama makamu wa rais kutoka mwaka 2006 hadi mwaka 2018 chini ya Rais wa zamani Ellen Johnson Sirleaf, na alitumikia taifa kwa zaidi ya miaka 40. Alishinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais mwezi Novemba, kwa 50.64% ya kura, dhidi ya 49.36% ya mpinzani wake, George Weah.
Atachukua madaraka wakati nchi hii ya Afrika Magharibi yenye wakaazi milioni tano, inayotafuta utulivu baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na janga la Ebola, inakabiliwa hasa na ufisadi na kiwango cha juu cha umaskini.
Matarajio makubwa
"Matarajio kwa uongozi wa Boakai ni makubwa kwa sababu ya uzoefu wake serikalini, sifa yake ya ustadi na mtu ambaye alijaribu kuishi kwa njia rahisi," amesema afisa wa zamani aliyechaguliwa katika Kaunti ya Nimba.
"Viongozi wote (wa Liberia) wameahidi kukabiliana na rushwa na kuboresha hali ya kiuchumi (ya watu) lakini wameshindwa kufanya hivyo. Yeye (Boakai) lazima afanye mabadiliko," amesema Abdulla Kiatamban, mchambuzi wa Geo Baraka group of strategists, kundi linalotoa ushauri.
Kwa upande mwingine, kushuka kwa bei ya bidhaa kama vile petroli na mchele kunatarajiwa, John Kollie, mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Liberia Media for democratic initiatives ameliambia shirika la habari la AFP. Mpito "laini na wa amani"
.Rais mteule alitoa wito kwa Waliberia "kuungana kama watu wamoja kujenga upya nchi yetu", katika taarifa nadra kwa umma mwishoni mwa mwezi wa Novemba, baada ya kuchaguliwa kwake. Aliahidi "kupanua maendeleo nchini kote", hasa kwa kujenga barabara katika eneo la kusini-mashariki, "zilizopuuzwa kwa miaka mingi".
Kama wakati wa kampeni yake, Bw. Boakai alikumbusha kuwa vita dhidi ya ufisadi vitakuwa mojawapo ya vita vyake na akadokeza kuwa ataweka mpango wa mpito "laini na wa amani". Pia alisema atafanya mageuzi ya "makali" ya usalama na haki na kutekeleza utawala wa sheria.
Kwa upande wake, Rais anayeondoka Weah, ambaye alimshinda Bw. Boakai mwaka wa 2017 katika duru ya pili, alikiri kushindwa kwake kabla ya ushindi wake kutangazwa rasmi, na kuvutia sifa za kimataifa.