Rais mustaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta na ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa Azimio alikosa kufika katika mkutano wa muungano huo uliofanyika katika hoteli ya Stoni Athi katika kaunti ya Machakos.
Ombi la kukosa kufika katika mkutano huo kutoka kwa Rais mustaafu iliwasilishwa na kinara wa Azimio Raila Odinga aliyesema kuwa Kenyatta anakubaliana na maamuzi yatakayoafikiwa katika mkutano huo.
"Ninaleta ombi la msamaha wa kutofika mkutanoni kutoka kwa mwenyekiti wetu Uhuru Kenyatta aliyetaka kuja lakini hakuweza japo amesema ataunga mkono maamuzi yoyote tutakayoafikia leo," Raila alieleza.
Raila alisema kuwa muungano huo ulikuwa katika matayarisho ya kuwatuma wawakilishi wake watakaowakilisha muungano huo katika mazungumzo ya kuleta maridhiano kati yao na wenzao wa Kenya Kwanza.
Kinara wa Azimio amesema kuwa watakao wawakilisha kama muungano wana jukumu la kuhakikisha kuwa matakwa yao ikiwemo kupungzwa kwa bei za bidhaa muhimu na ukaguzi wa sava zilizotumika katika uchaguzi uliopita zinashughulikiwa.
Kiongozi wa KANU Gideon Moi pia alikosa kufika katika mkutano huo lakini alituma mwakilishi wake katika mkutano uliowajumulisha viongozi waliochaguliwa chini ya muungano wa Azimio.
Raila amesema kuwa iwapo watakosa kuafikiana na Kenya Kwanza kuhusu matakwa yao basi hawatakuwa na budi ila kurejelea katika maandamano ili kuishurutisha serikali kuangazia matakwa hao.