Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Kagame, Nyusi kuwakabili waasi wa Msumbiji

Rwanda Kgm Rais Kagame, Nyusi kuwakabili waasi wa Msumbiji

Sun, 26 Sep 2021 Chanzo: mwananchidigital

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameanza ziara ya siku mbili nchini Msumbiji ambako amepeleka wanajeshi 1,000 kwa ajili ya kusaidia kudhibiti wanamgambo wa Jihad wanaofanya vitendo vya kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.

Kiongozi huyo na mwenyeji wake Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, walitarajiwa kukutana na na waandishi wa habari jana jioni kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano wa mataifa hayo mawili, ikiwemo suala la usalama.

Rwanda imekuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kuitikia wito wa kuisaidia Serikali ya Msumbiji iliyoomba msaada wa kuongezewa nguvu za kijeshi na vifaa kwa ajili kupambana na wanamgambo hao wanaohusishwa na kundi la kiggaidi la Islamic State (IS).

Julai mwaka huu, Rais Kagame aliwaaga wanajeshi wa nchi hiyo walioondoka kwenda Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado lenye utajiri wa gesi.

Kabla ya hatua hiyo ya Rwanda, mara kwa mara wanajeshi wa Msumbiji walikuwa wakipambana na wanamgambo hao wa Jihad ambao wamekuwa wakiua na kuteka watu, kupora mali, kuharibu mali na kuvamia maeneo mbalimbali, hali iliyosababisha wakazi wa maeneo husika kukimbia nyumba zao.

Rais Kagame aliwasili kwa ndege katika jimbo la Pemba jana asubuhi na mambo atakayofanya katika ziara hiyo ni kukutana na kufanya mazungumzo na vikosi vya jeshi na polisi vilivyopelekwa Cabo Delgado kulinda amani.

Vikosi vya kigeni vimesaidia Msumbiji kuendelea kulinda ardhi yake tangu wanamgambo walipoanzisha shambulio lililoratibiwa katika mji wa bandari wa Palma mwezi Machi, mwaka huu na kusababisha wasiwasi katika eneo ambalo linatekelezwa miradi ya gesi.

Shambulizi hilo lilifanya jumuiya za kimataifa kuhofia kukwama kwa miradi ya gesi ya mabilioni ya dola sambamba na kuwaweka roho juu watu wanaoishi maeneo yaliyoshambuliwa.

Mbali na Rwanda, wanachama 16 wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) pia zimepeleka majeshi yao, huku mataifa jirani na Msumbiji yameahidi kupeleka wanajeshi 1,500.

Umoja wa Ulaya nao wamesema wanaandaa mpango madhubuti wa kuisaidia Msumbiji kwa kuwapa mafunzo ya kijeshi wanajeshi ili wawe na mbinu za kisasa kukabiliana na ugaidi.

Chanzo: mwananchidigital