Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raila awapasua kichwa wanasiasa urais 2022

1b48d5bcdcd3833d32a32e8979f22677.jpeg Raila awapasua kichwa wanasiasa urais 2022

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI wa upinzani nchini Kenya anayeongoza chama cha ODM, Raila Odinga, anasumbua vichwa vya wanasiasa wengi nchini humo, hasa chama tawala cha Jubilee, juu ya ikiwa atagombea au hatagombea nafasi ya urais mwaka 2022.

Kwa muda mrefu kiongozi huyo amekuwa kimya bila kuweka wazi nia yake kwa umma kuwa atagombea au la.

Ukimya huo umekuwa shubiri kwa wanasiasa wengi hata wa upande wa upinzani, kwani wanashindwa kujipanga kwa sababu wanahofia kivuli chake.

Lakini matamshi ya mwanachama wa chama tawala cha Jubilee ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Jubilee na mtu wa karibu wa Rais Kenyatta, Francis Atwoli, yanaonekana kuchochea moto wa siasa nchini humo.

Atwoli ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Kikuu cha Wafanyakazi Kenya (COTU), hivi karibuni alisema hadharani kuwa, katika siasa za nchi hiyo, mtu pekee ambaye anaweza kumshinda Naibu Rais, William Ruto ni Odinga bila kujali chama.

"Ikiwa kuna mtu ambaye anaweza kumsimamisha huyu mtu (Ruto) kutokuwa Rais, ni aliyekuwa Waziri Mkuu (Odinga). Hakuna mwingine yeyote," Atwoli amekuwa akinukuliwa akisema mara kwa mara katika vikao vya Jubilee.

Itakumbukwa, Ruto alikuwa akiandaa mikutano mingi ya kisiasa ambayo wengi walioona kama yenye kujitafutia umashuhuri na jukwaa la kisiasa kwa ajili ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Hivi karibuni Atwoli na Seneta wa Siaya, James Orengo, wamekuwa wakitoa matamshi ya kumuunga mkono Odinga kugombea urais na kudai kuwa, Rais Kenyatta na kiongozi huyo wa upinzani walikuwa wakiunda muungano ambao ungepelekea kinara huyo wa ODM kupambana na Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Chanzo: habarileo.co.tz