KIONGOZI wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, ametoa mwito kwa viongozi wa kisiasa nchini humo kuepuka kutoa kauli za uchochezi kwa wananchi na badala yake wajenge hoja za kuwaunganisha Wakenya ili kudumisha amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na viongozi kutoka Jimbo la Kajiado juzi, kiongozi huyo alisema taifa hilo lina historia mbaya ya vurugu, hivyo kuna haja ya kuwapo mshikamano na amani wakati serikali ikikabiliana na janga la covid-19.
“Natoa mwito kwa viongozi kusimamia umoja wa taifa na kuwapuuza viongozi wanaohubiri chuki dhidi ya Wakenya. Taifa hili lina historia ya vita kwa sababu ya siasa. Hakuna anayestahili kulirejesha taifa hili kwenye vita kwa sababu ya siasa,” alisema.
Odinga aliwasihi wananchi wa Kenya kuwaheshimu viongozi wao kuanzia Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, kutokana na mchango wao mkubwa katika kulijenga taifa hilo.
“Kutoa lugha chafu hakuhalalishwi na hasira kutoka kwa viongozi hasimu wa kisiasa, bali kinachotakiwa ni kuvumiliana na kusameheana ili kujenga taifa lenye umoja wa kitaifa,” alisema.