Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ameelezea kuhusu jukumu la Rais Uhuru Kenyatta katika azma yake ya kuwania urais 2022Raila ametetea nia yake ya kuwania urais 2022 akisema kwamba yeye sio mradi wa mtu yeyote
Raila alizidi kusema kuwa yeye haitaji kuidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta, kwenye kinyang'anyiro cha Ikulu mnamo Agosti 2022, ila anahitaji ampigie kuraKinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, ametetea azma yake ya kuwania kiti cha urais 2022 akisema kwamba yeye sio mradi wa mtu yeyote.
Akizungumza siku ya Jumatano Disemba 29, kwenye mahojiano ya runinga, Raila alizidi kusema kuwa yeye haitaji kuidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta, kwenye kinyang'anyiro cha Ikulu mnamo Agosti 2022.
"Mimi sitaki kuidhinishwa na Uhuru Kenyatta. Ninataka kura yake. Ikiwa Raia atanipigia kura, nitashukuru sana. Mimi sio mradi wake na mimi sitaki kuwa mradi wake." Raila alisema.
Waziri mkuu huyo wa zamani alisema kwamba yeye ametosha kuliongoza taifa la Kenya.
Huku akiorodhesha mafanikio yaliyoafikiwa humu nchini yangu Kenya ijinyakulie uhuru wake, Raila alisema nchi hii inahitaji mhandisi atakayeipeleka kwenye upeo katika nyanja za kimataifa hususan kimaendeleo.
"Mimi ninatosha kuliongoza taifa hili hadi kufikia kiwango cha juu. Kenya inahitaji mhandisi ndipo iweze kufanana na mataifa mengine katika maendeleo tangu ijinyakulie uhuru mwaka wa 1963. Tukiwa na juhudi za pamoja, nitaweza kutambua vipaji katika nyanja tofauti ili taifa letu lisonge mbele," Raila aliongeza kusema.
Waziri mkuu huyo wa zamani alimpa heko rais wa kwanza wa taifa hili hayati mzee Jomo Kenyatta kwa kulikomboa nchi hii kujinyakulia uhuru, Daniel Moi kwa kuimarisha elimu, Mwai Kibaki kwa ruwaza ya maendeleo ya 2030 na Uhuru Kenyatta kwa miundo misingi.