Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raila: Msipeleke tamaa bungeni

Railaa Msipeleke tamaa bungeni

Sun, 18 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amewaonya wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja dhidi ya kuonyesha ubinafsi bungeni na kupigania nyadhifa mbalimbali katika Serikali.

Akizungumza juzi Ijumaa Septemba 16, 2022 baada ya kukutana na wabunge wa muungano huo Kaunti ya Machakos, Odinga aliwataka wabunge wake waungane na kutumia idadi yao bungeni kuleta mabadiliko nchini.

Alisema kuwa muungano huo unawategemea wabunge hao hasa katika kuleta mabadiliko katika Mahakama ya Juu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC).

“Msipigane vita miongoni mwenu. Tuko katika muungano wa Azimio na kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa sote ni kitu kimoja. Usipoteuliwa katika wadhifa fulani, usimchukie mwenzako. Tuungane ili pamoja tusonge mbele,” akasema Odinga.

“Kikao hiki kiliandaliwa ili kuwaunganisha wajumbe wetu na kuwahimiza walinde maslahi yetu kama muungano bungeni. Msipoungana, basi mtatawaliwa bungeni,” amesisitiza Odinga.

Kwa upande mwingine, Odinga alisema kuwa jukumu la wabunge litakuwa kutekeleza majukumu matatu.

“Bunge linafaa kuiokoa idara ya Mahakama ambayo imetekwa nyara na Serikali tawala, kubadilisha tume ya IEBC na kuwaokoa wananchi dhidi ya uongozi mbaya,” akasema Odinga.

“Bunge lazima lisimame dhabiti na kuvilinda vyama vyetu vya kisiasa. Tuna jukumu kama Azimio kuchukua madaraka na kutumia idadi yetu Bunge kuhakikisha kuwa wananchi wanatumikiwa ipasavyo.”

Kwa upande wake, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua aliwahimiza wabunge wa Azimio kuungana ili kuepuka kutawaliwa na mrengo wa Kenya Kwanza.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alishindwa na mpinzani wake, William Ruto ambaye alitangazwa kuwa Rais wa taifa hilo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9 mwaka huu.

Hata hivyo, Odinga alifungua kesi kupinga ushindi wa kiongozi wa Kenya Kwanza, Ruto aliyetangazwa mshindi wa urais Agosti 15, 2022 na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika matokeo yaliyotangazwa na IEBC, Dk Ruto ambaye kati ya 2013 na 2022 alihudumu kama naibu wa Rais, alipata kura 7,176,141 kiwango kinachowakilisha asilimia 50.49 ya idadi jumla ya kura zilizopigwa huku Raila akipata kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85.

Baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kusikiliza kesi hiyo, Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Martha Koome alitupilia mbali kesi hiyo, akisema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.

Septemba 13 mwaka huu, Dk William Ruto aliapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya akichukua nafasi ya Uhuru Kenyatta ambaye alimaliza muda wake wa miaka 10.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz