Wakati wakili Julie Soweto anayemtetea kiongozi wa Umoja wa Azimio, Raila Odinga akidai raia wa Venezuela ndiye aliyeamua nani Rais wa Kenya, mawakili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wameiambia mahakama nyaraka zinazowasilishwa na mawakili wa Odinga ni za kughushi.
Juzi Ijumaa Septemba 2, 2022 ilikuwa siku ya mwisho kwa mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, wanaoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, katika kesi ya kupinga ushindi wa urais wa mgombea urais kupitia chama cha UDA, Dk William Ruto.
Ruto alitangazwa mshindi na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kwa kupata asilimia 50.49 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Odinga aliyepata asilimia 48.85. Jumatatu mahakama hiyo itatoa uamuzi wake.
Kabla ya wakili Soweto kujieleza mbele ya mahakama, wakili mwenzake, Paul Mwangi alisisitiza kuwa raia wa Venezuela, Camargo Camargo aliacha alama za vidole vyake kwenye fomu hizo.
Hata hivyo, mawakili wa IEBC walikanusha madai hayo ya upande wa walalamikaji ya mkono wa raia huyo wa Venezuela kwenye uchaguzi wa rais.
Kulingana na wakili, Mahat Somane, raia hao wa Venezuela Camargo, Joel Gustavo Rodriguez Garcia na Salavador Javier Suarez walipewa nafasi maalumu ya kuingia kwenye seva, lakini hawakuwa na uwezo wa kusababisha hila.