Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raia wa Sudan wazidi kuyakimbia mapigano

Watu Zaidi Ya Laki Moja Kutoka Sudan Wameingia Chad Raia wa Sudan wazidi kuyakimbia mapigano

Mon, 26 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanamgambo wa kundi la RSF la nchini Sudan, wanasema wanakishikilia kituo kikubwa cha polisi kilichokuwa na silaha nzito wakati wa mapiganao makali baina yake na jeshi huku watu takribani 12 wakiuawa mjini Darfur.

Katika taarifa yake, kundi la wanamgambo la RSF, limesema kwamba limechukua udhibiti kamili wa kituo cha polisi wa akiba kusini mwa Khartoum na kuchapisha video za wapiganaji wake wakisherehekea ndani ya kituo, baadhi wakiondoa masanduku ya risasi kutoka kwenye ghala. Tangu Jumamosi jioni mapigano yameripotiwa kuongezeka katika miji mitatu ya Khartoum, Bahri na Omdurman huku mzozo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF ukiingia wiki ya 11.

Mashuhuda wameripoti pia ongezeko la machafuko kwenye mji mkubwa wa Nyala katika mkoa wa magharibi wa Darfur kama anavyosimulia raia huyu wa Sudan; "Tunatumai kuwa vita hivi vitaisha. Watu wameumizwa vibaya sana kutokana na vita hivi. Baadhi wamekimbia nyumba zao na wengine wamekwama mipakani. Tunaamini kwa msaada wa Mungu vita hivi vitakomeshwa.”

Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari siku ya Jumamosi kwamba ghasia za Darfur zimechukua "mwelekeo wa kikabila" na zinaweza kujumuisha "uhalifu dhidi ya ubinadamu", na kuonya juu ya mauaji ya watu kutoka jamii ya Masalit katika eneo la El Geneina Darfur Magharibi. Khartoum na El Geneina ni maeneo yaliyoathirika vibaya na vita, ingawa wiki iliyopita mapigano yalienea katika maeneo mengine ya Darfur na Kordofan upande wa kusini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live