Viongozi wa Sudan Kusini wamesisitizwa kufanyia kazi ombi la Papa Francis la kuleta amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya muda mrefu.
Papa alifanya "hija ya amani" nchini humo mwishoni mwa juma akiwa na wakuu wa makanisa wa nchini Uingereza na Scotland.
Katika mahubiri yake ya Jumapili wakati wa misa katika mji mkuu wa Juba, Papa aliitaka nchi hiyo kukataa "sumu ya chuki".
Raia wa Sudan Kusini wana matumaini kuwa viongozi wao watazingatia ushauri huo.
"Natarajia viongozi wetu kubadilisha mioyo yao na kutekeleza ujumbe wa amani ulioletwa na Papa Francis ili watu wa Sudan Kusini wawe na amani ya kudumu," Imma Lasu aliiambia BBC baada ya misa.
Rose Adao, muumini wa Kanisa la Pentekoste, alisema anawataka viongozi wa Sudan Kusini watubu na kutekeleza ujumbe wa amani ulioletwa na Papa Francis.
Elisabeth Mayak Thomas mwenye umri wa miaka 20, alikuwa miongoni mwa waliojitolea katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Papa. Alisema anatarajia viongozi "kutekeleza makubaliano ya amani na kupatanisha watu wetu".