Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raia wa Rwanda wapo salama-Ripoti

Df5ab9aa4c1c6fe4be9a687af91a83be.png Raia wa Rwanda wapo salama-Ripoti

Tue, 15 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RIPOTI ya kitaifa ya utawala bora imeonesha kuwa, raia wa Rwanda wako salama kwa asilimia 95.44.

Bodi ya Utawala ya Rwanda (RGB) imetoa ripoti hiyo hivi karibuni inaonesha kuwa kiashiria cha usalama kinabaki kuwa nguzo inayofanya vizuri zaidi ya viashiria vyote vilivyopimwa.

Katika eneo hilo toleo lililopita lilipata asilimia 94.29.

Ripoti hiyo imepima kiwango cha usalama ikiwamo usalama binafsi na mali, upatanisho, mshikamano wa kijamii, umoja wa kitaifa na jinsi usalama wa kitaifa unavyolindwa.

Raia wa nchi hiyo wameonesha uaminifu kwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda kwa kiwango cha asilimia 99.23, huku polisi wakipata asilimia 90.88.

“Linapokuja suala la usalama wa kibinafsi na mali asilimia 87.10 wanajisikia salama kutembea usiku peke yao wakati asilimia 81.90 wamebainisha kuwa mali zao ni salama na asilimia 92.51 wanahisi kuridhika na usalama wao wa binafsi,” ilisema ripoti hiyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa RGB, Usta Kaitesi alisema wanafanya hivyo kwa sababu wanataka uwajibikaji, uwazi na kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa maslahi ya raia.

Nguzo ya ushiriki na ushirikishaji wananchi ilipata kiwango cha juu zaidi cha uboreshaji kwa asilimia 8.96 ikilinganishwa na toleo lililopita, uboreshaji huo umetokana na uboreshaji wa utendaji kazi na ushiriki wa raia ambao ulipata asilimia 82.53 kutoka asilimia 72.68 katika toleo lililopita.

Utendaji wa serikali za mitaa ulipata asilimia 81.31 dhidi ya asilimia 70.70 iliyopatikana katika toleo lililopita, huku kuwekeza katika maendeleo ya binadamu na jamii ndio nguzo iliyofanya vibaya zaidi kwa kupata alama asilimia 73.32.

Chanzo: habarileo.co.tz