Wakati wananchi wa Ethiopia kote ulimwenguni wakitumai kwamba mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya serikali na TPLF utaendelea kuheshimiwa, baadhi yao Jumatatu wamekutana kwenye ofisi za VOA, Washington DC, katika kikao cha mazungumzo kuhusu suala hilo.
Kikao hicho kilichopewa jina, Ethiopia:Paths to Peace, na ambacho kilirushwa kwa njia ya televisheni, kiliwaleta pamoja wanaharakati, wasomi pamoja na watu kutoka makabila mbali mbali ya Ethiopia, wakizungumzia mzozo wa miaka miwili, uliokuwa karibu kulisambaratisha taifa lao.
Wengi wa waliohudhuria walikubaliana kwamba vikao vya aina hiyo ni muhimu katika kurejesha amani nchini humo. Meaza Gebremedhin ambaye ni mwanaharakati wa Tigary, mtafiti pamoja na mwanaharakati wa haki za binadamu, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria kikao cha jana, na tangu vita vya Tigray kuzuka, amekuwa akipanga maandamano ya kulalamikia ukatili uliokuwa ukiendelea nchini mwake.
Ripoti zinasema kwamba kutokana na juhudi zake, amewahi kutishiwa maisha kwa bunduki kwenye mkutano mjini Los Angeles, lakini anasema kwamba hilo halitishi zaidi ya ukatili unaoendelea nchini Ethiopia.