Watu karibu 3,000 wameuawa huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa (NGOs) na kueleza kuwa, watu 2,750 wameuawa katika majimbo yenye migogoro mikubwa mashariki mwa DRC ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.
Taasisi hiyo yenye mashirika 124 ya kimataifa nchini DRC imesisitiza kuwa, kuna haja kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo hayo wanafikiwa na misaada ya kibinadamu.
Taarifa yajukwaa hilo imesema uwepo wa makundi ya waasi wanaobeba silaha katika maeneo hayo ya mashariki mwa DRC umepelekea mamilioni ya wakazi kuyahama makazi yao, na hivyo kushadidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo inashuhudiwa katika maeneo hayo kwa miaka mingi sasa.
Wakimbizi katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa DRC
Takwimu zilizotolewa Jumatatu iliyopita na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) zinaonesha kuwa, watu milioni 2 na laki 8 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mwezi Machi 2022 huko mashariki mwa Kongo DR.
Kadhalika unyanyasaji wa kijinsia umekithiri huku kesi zaidi ya 31,000 zikiwa zimesajiliwa katika miezi mitatu ya kwanza ya 2023 pekee mashariki mwa DRC.