Shirika la ndege la Qatar limetangaza kusitisha safari zake za kuelekea Sudan kutokana na kufungwa kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum, Shirika la Habari la Qatar lilisema Jumapili.
Mapigano yalizuka siku ya Jumamosi kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza la Utawala la mpito la Sudan, na Kikosi cha wanamgambo cha RSF, kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, ambaye ni naibu mkuu wa baraza hilo.
Wanajeshi na RSF walidai kuwa wanadhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum na mitambo mingine muhimu ambapo mapigano yalizuka usiku kucha.
Mapigano hayo yamezuka katika mji mkuu, Khartoum, na kwingineko nchini humo ni matokeo ya moja kwa moja ya mvutano mkali wa madaraka ndani ya uongozi wa kijeshi wa Sudan.
Tangu mapinduzi ya Oktoba 2021, nchi imekuwa ikiendeshwa na baraza la majenerali - na kuna wanajeshi wawili katikati mwa mzozo huo.