Viongozi na maafisa wa baraza la mji wa kisiwa cha Lamu nchini Kenya wamelalamikia tabia ya wafugaji wa punda kuwaachilia wanyama hao kuzurura hovyo mtaani na kuleta kero kwa wananchi ambapo pia baadhi ya wanyama hao hukimbizana hovyo na kuishia kufanya matendo ya aibu yanayowafunza watoto tabia mbaya.
Diwani wa eneo hilo ya Shella Atwa Salim, aliweka wazi kuwa kamwe hapendezewi na tabia ya punda wanaorandaranda mitaani, kufukuzana ovyo vichochoroni na majumbani, ambapo huishia kujamiiana hata mbele ya watoto.
Bw Salim anasema kamwe hataruhusu maadili ya jamii ya Lamu, hasa wakazi wanaoishi mji wa kale wa Lamu na Shella kupotoshwa kupitia vitendo vya hayawani hao.
“Punda warandaji wamekuwa kero kwa masikio yetu na hata kimaadili. Unapata punda wanapiga kelele kila mahali usiku na mchana na kutukosesha amani. Wengine wanafukuzana na kisha kujamiiana hadharani huku watoto wa shule na wale wachanga wakitazama. Hilo linaleta fikra potofu kwa kizazi chetu kichanga. Lazima mikakati kabambe iwekwe kudhibiti hawa hayawani,” alisema Bw Salim.