Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa Mkenya amlilia JPM

85d1fe807a4e49a08ef6bd26eabcb03f.png Profesa Mkenya amlilia JPM

Sun, 28 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

PROFESA wa Sheria na Mtoa Mihadhara Maarufu kutoka Kenya, Patrick Lumumba amesema majonzi, simanzi na vilio vilivyooneshwa na Watanzania wakati wa mazishi ya Rais John Magufuli vimedhihirisha alikuwa ni mtu wa kipekee na mwenye matendo mema kwa taifa lake.

Profesa Limumba amesema Rais Magufuli ni mmoja wa viongozi wachache Afrika waliokuwa na wazo la kuiokomboa Afrika kutoka kwenye kiini cha ukoloni mamboleo.

Aidha, ameonesha kusikitishwa na namna baadhi ya watu wanaojiita wapinzani ambao hata baada ya kifo cha kiongozi huyo, wameendelea kutoa maneno ya hovyo dhidi yake jambo ambalo ni kinyume cha mila na tamaduni za Kiafrika.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua maradhi ya hitilafu umeme wa moyo.

Lumumba mwenye umri wa miaka 59, wasifu wake unaonesha aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kupambana na Rushwa ya Kenya mwaka 2010 hadi Agosti 2011 na sasa ni Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya tangu mwaka 2014.

Katika video ya kumuomboleza Magufuli, Profesa Lumumba alisema alibahatika kuzungumza na Rais Magufuli na kwamba, alikuwa kiongozi mwenye maono ya kuikomboa Afrika katika ukandamizaji.

“Ikiwa kuliwahi kuwa na mkuu wa nchi wa Tanzania aliyekuwa na maono na mitazamo ya Mwalimu Julius Nyerere, basi alikuwani John Magufuli,” alisema Profesa Lumumba.

Alimtaja Magufuli kuwa kiongozi myenyekevu, mwenye kujitolea, Mtanzania na Mwafrika mzalendo wa kweli.

Alisema pamoja na Tanzania na Afrika kumpoteza kiongozi huyo bora, kwa sasa mitandaoni kumejaa wanadharia na kusisitiza kuwa anakataa kuogelea katika bahari ya njama kwa sababu imejaa mamba na kiboko ambao hataki kukaa nao.

“Ninachagua kutembea kwenye uwanja thabiti ambao JPM alijenga wakati akiishi hapa duniani. Swali lililobaki kwangu mimi na wewe kujiuliza na kujijibu, je tumejifunza nini kwa mtu kama Dk John Magufuli?” alisema.

Alisema tangu alipoingia Ikulu, Rais Magufuli alitambua kuwa ofisi hiyo ni fursa kwake kuwatumikia wanyonge na kufanya mema kwa kuwa ni vyema na muhimu kuwatendea wengine mazuri.

“JPM kwa sasa upo mbinguni na natamani niamini kuwa yupo upande mzuri wa historia. Majonzi, simanzi na vilio vilivyooneshwa na Watanzania wakati wa mazishi yake vilionesha kuwa alikuwa ni mtu wa kipekee na alikuwa na matendo ya kipekee,” alisema Profesa Lumumba.

Kwa mujibu wa Profesa Lumumba, watu wengine wakiwamo Watanzania waliobaki duniani wanapaswa kujiuliza watafanya mambo gani kumuenzi Magufuli na namna watakavyomkumbuka.

“Nakumbuka siku moja nilikaa naye kwa saa moja tukizungumzia Afrika hivyo ndivyo watu wengi sasa wanazungumzia kiongozi huyo sasa iwe ni kweli au uongo kuwa walizugumza naye, huu ni wakati wa kusherehekea maisha ya kiongozi huyo bora kabisa,” alisisitiza.

Alisema wengi wanaweza wakawa hawajawahi kufika mitaa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Kigoma na Mtwara, lakini yeye amebahatika kufika katika miji hiyo na kujionea namna kiongozi bora anaweza kufanya kutumikia taifa lake.

Katika mihadhara yake mara kadhaa, Profesa Lumumba amesikika akimzungumzia Dk Magufuli kuwa ni kiongozi wa mfano huku akisifia aina ya utendaji na uongozi wake.

Dk Magufuli alizikwa juzi kijijini kwao Chato, katika maziko yaliyofanyika kijeshi huku yakihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, kimataifa, mabalozi, wasanii, familia na wananchi mbalimbali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz