Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa Lwaitama amjibu Wasira kuhusu maandamano

Lwaitamaaaa.jpeg Profesa Lwaitama amjibu Wasira kuhusu maandamano

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na kauli za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Stephen Wasira za kukosoa tangazo la Chadema kuandaa maandamano Januari 24, mwaka huu kupinga miswada ya sheria za uchaguzi, chama hicho kimemjibu kikitaka asome vizuri tamko la maandamano hayo.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza vuguvugu la kudai haki litakaloambatana na maandamano ya amani kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu.

Miswada hiyo ni wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili Januari 17, mwaka huu, Wasira pamoja na mambo mengine alihoji sababu ya Chadema kupanga kufanya maandamano kabla ya kusubiri Bunge kujadili maoni ya wadau na kupitisha sheria.

“Sasa mimi nauliza, Bunge halijamaliza kazi yake ya kuchakata maoni, litakutana mwezi ujao na Mbowe anaitisha maandamano Januari 24, siku chache kabla ya Bunge, halafu anasema maoni ya wananchi yamekataliwa, yamekataliwaje wakati hawajamaliza?” alihoji Wasira.

Akizungumzia kauli za Wasira, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Profesa Azaveli Lwaitama amesema kada huyo wa CCM hajaelewa lengo la chama hicho kuandamana.

“Mwenyekiti (Mbowe) ameeleza kuwa, jinsi kamati ilivyoyapokea mapendekezo ya Chadema kupitia wasilisho la Katibu Mkuu, John Mnyika ilionyesha mwelekeo wa kuyakataa yote matatu ya msingi ya chama hicho,” amesema.

Ameyataja mapendekezo hayo kuwa ni Chadema kutaka Bunge liiombe Serikali iitoe miswada hiyo mitatu bungeni na badala yake iletwe kwanza bungeni miswada miwili.

Alisema, “Pendekezo la pili la Chadema ni kuwa kwa sasa Serikali ipeleke bungeni kwanza muswada wa kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.”

“Huu ndiyo muswada utakaounda vyombo vya kimuafaka vya kusimamia kukamilishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya,” amesema.

“Vyombo hivi ni kama vile jopo la wataalamu ambalo litapendekeza maudhui ya Katiba mpya ikiwa ni pamoja na vifungu pendekezwa kuhusu masuala ya uchaguzi, Tume ya Uchanguzi na usajili wa vyama vya siasa,” amesema.

Amesema suala la kuundwa kwa jopo la wataalamu ni pendekezo la kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala.

“Chadema kimeafiki pendekezo hilo, lakini kimependekeza kuwepo pia Tume ya Maridhiano (reference group) na mkutano mkuu au Bunge la Katiba),” amesema.

Kuhusu pendekezo la tatu, amesema chama hicho kinaitaka Serikali ipeleke baadaye kidogo muswada wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba ya sasa kuhusu masuala ya uchaguzi, Tume ya Uchaguzi na usajili wa vyama vya siasa.

“Muswada huu wa pili kati ya miwili inayopendekezwa na Chadema iletwe bungeni baada ya kuanza kufanya kazi kwa vyombo vya kimuafaka vya kusimamia kuandikwa kwa Katiba mpya (hususani jopo la wataalamu).

“Hivyo ndivyo vitakuwa vyombo sahihi vya kujenga muafaka wa kitaifa kuhusu maudhui ya Katiba mpya pendekezwa ikiwa ni pamoja na masuala ya uchaguzi, Tume ya uchanguzi, na usajili wa vyama vya siasa,” amesema.

Amesema mapendekezo hayo matatu ya msingi ya Chadema yalizuiwa kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge kwa mdomo, badala yake ikamwelekeza Katibu Mkuu wa chama hicho, Mnyika awasilishe yale ya kifungu kwa kifungu.

“Kwa kweli Kamati iliweka wazi kuwa haikuwa tayari kupokea mawazo ya wadau yaliyogusia kutanguliza mabadiliko madogo ya Katiba ya sasa kabla ya kuzungumzia maudhui ya miswada mitatu ilivyokuwa mbele ya Bunge,”amesema Profesa na kuongeza:

“Maandamano ni njia sahihi ya kushinikiza Kamati ya Bunge kupendekeza kuwa Bunge litakalokaa mwezi ujao analolitaja Wasira liitake Serikali kuiondoa bungeni hii miswada mitatu. Maandamano baada ya Bunge kukaa yatakuwa hayana maana.”

Amesema msingi wa maandamano ni kuwa Bunge likikaa na kamati ikawa haikupendekeza Serikali iiondoe miswada hii bungeni, basi Serikali yenyewe iiondoe kwa kushinikizwa na maandamano.

“Lengo la maandamano ni kushinikiza Serikali kuiondoa miswada hii na isipelekwe bungeni kujadiliwa, badala yake muda wa kikao cha Bunge utumiwe vizuri kujadili hatua mahususi za Serikali kukabili suala la ugumu wa maisha,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live