New Delhi. Maelfu ya watu wamekamatwa na polisi katika maeneo tofauti ya India baada ya kukiuka marufuku ya kuandamana dhidi ya sheria mpya ya uraia.
Polisi walitumia virungu na gesi ya kutoa machozi kutawanya umati wa waandamanaji na wengine kutiwa mbaroni.
Ghasia ziliibuka katika mitaa ya Lucknow, mji mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh, ambako waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe walikabiliana na polisi na kuchoma magari. Ghasia nyingine zimeripotiwa katika mji wa Gujarat.
Kwingineko maandamano yalifanyika kwa amani huku maelfu ya watu wakikamatwa na kushushwa kutoka kwenye mabasi.
Amri ya kuzuia mikusanyiko mikubwa ilitolewa katika miji kadhaa ya India. Maandamano hayo yanahudhuriwa kiasi kikubwa na wanafunzi, asasi za kiraia na vyama vya upinzani.
Sheria inayopingwa inalenga kutoa uraia kwa wahamiaji haramu kutoka katika madhehebu sita ya dini, wakiwamo wa Wahindu, Wasikhi, Wabudda, Wajain, Parsi na Wakristo kutoka Afghanistan na Pakistan, lakini sheria hiyo inawazuia wahamiaji Waislamu kuomba uraia.
Vyama vya upinzani na asasi za kiraia vinasema sheria hiyo ni kinyume kanuni za masuala ya dini zilizomo katika Katiba ya India kwa kuwa inawabagua Waislamu.
Kesi sita zimefunguliwa katika mahakama kuu kupinga sheria hiyo.