Vijana 21 walifariki mwishoni mwa juma baada ya burudani ya usiku kwenye kilabu cha pombe katika kitongoji kimoja nchini Afrika Kusini, maafisa wamesema Jumapili.
Ingawa chanzo cha vifo hivyo bado hakijabainika, maafisa wa eneo hilo na wanasiasa wamesema wanahofia huenda ikawa ni kisa cha unywaji pombe kwa vijana wenye umri mdogo ambao ulisababisha msiba huo.
Gavana wa mkoa wa Eastern Cape amesema wasichana wanane na wavulana 13 walifariki kwenye kilabu hicho cha pombe, katika eneo la makazi liitwalo Scenery Park. 17 walikutwa wamekufa kwenye eneo la tukio, huku wengine wakifia hospitalini.
Chupa tupu za pombe, wigi na hata bango dogo la rangi ya zambarau lenye maandishi “ Happy Birthday” vilikutwa vimetapakaa kwenye barabara yenye vumbi nje ya ghorofa mbili za kilabu hicho kiitwacho Enyobeni Tavern, amesema Unathi Binqose, afisa wa serikali anayehusika na usalama aliyefika kwenye eneo la tukio nyakati za alfajiri.
Waathiriwa wengi wanaaminika kuwa wanafunzi waliokuwa wanasherekea kumalizika kwa mitihani ya shule yao ya sekondari Jumamosi usiku, maafisa wamesema.
Hakuna majeraha yaliyoonekana kwenye miili ya waliokufa, lakini uchunguzi wa maiti utabaini ikiwa vifo hivyo vinaweza kuhusishwa na sumu, wameongeza.