Polisi wa zamani wa Burundi Spiros Richard Hagabimana anataka kuwa mbunge wa kwanza Mgiriki mweusi, katika nchi ambako wahamiaji ni nadra kushikilia nyadhifa za umma.
Anagombea kiti cha ubunge cha wilaya ya kusini – mashariki ya Piraeus II kwa tiketi ya chama cha kihafidhina cha New Democracy, katika uchaguzi wa tarehe 21 Mei.
"Piraeus ni mahala ambapo nilisomea, nilijifunza maneno ya kwanza ya Kigiriki, kufanya kazi na kuishi. Kupitia eneo hili, nilijifunza kuipenda Ugiriki," moja ya mabango ya uchaguzi ya Bw Hagabimana liliandikwa kwenye ukurasa wa Twitter.
Habimana mwenye umri wa miaka 54-ameliambia shirika la habari la Reuters jinsi alivyofungwa alipokuwa afisa wa polisi nchini Burundi mwaka 2015 kwa kukataa kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali.
Baadaye aliachiliwa huru kutoka gerezani kwa usaidizi wa maafisa wa Ugiriki na kurejea Athens mwaka 2016.
Bw Hagabimana aliwasili Ugiriki mwaka 1991 kwa ajili ya masomo katika shule ya mafunzo ya jeshi la majini. Alihitimu mwaka 1996 lakini alilazimika kuomba ukimbizi nchini Ugiriki kwani Burundi wakati huo ilikuwa katika mzozo wa mapinduzi ya kijeshi, kulingana na ripoti za Reuters.
Alipata uraia wa Ugiriki mwaka 2005 na katika mwaka huo huo alirejea Burundi kwa ajili ya juhudi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Alisema kuwa rangi ya ngozi yake haipaswi kuagaziwa katika uchaguzi ujao.