Aliyekuwa mgombea urais wa Uganda na kiongozi wa upinzani Kizza Besigye amezuiwa kuondoka nyumbani kwake alipokuwa akijaribu kuanzisha maandamano dhidi ya serikali kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.
Polisi walizingira nyumba ya mpinzani huyo huko Kasangati, kitongoji kilicho umbali wa kilomita 12 kutoka mji mkuu, Kampala.
Msemaji wa Polisi wa Jiji la Kampala Luke Owoyesigire alisema polisi walimzuia Dk Besigye kuondoka nyumbani kwake kwa sababu wanaamini maandamano yaliyopangwa katikati mwa jiji yangegeuka kuwa ya fujo kama wangeruhusiwa kuendelea.
Alisema mwanasiasa huyo pia hajafuata miongozo chini ya Sheria ya Usimamizi wa Maadili ya Umma, sheria inayosimamia mikusanyiko ya watu nchini.
Polisi sasa wametumwa kuweka ulinzi karibu na nyumba ya Dkt Besigye hadi ilani nyingine.