Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi adaiwa kumvuja mkono mwananchi kisa amegoma kumnunulia pombe

Mkono Polisi Polisi adaiwa kumvuja mkono mwananchi kisa amegoma kumnunulia pombe

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Polisi mmoja katika Kaunti ya Murang’a anachunguzwa kwa madai kwamba alimjeruhi mwanamume aliyekuwa akitembea kwa miguu akielekea nyumbani Desemba 13, 2023.

Baadhi ya wakazi wanadai kwamba afisa huyo alikuwa awali amemtaka mwanamume huyo kumnunulia pombe lakini alipokataa, akamuonya angemwadhibu akielekea nyumbani kwa “kosa la kukataa kuburudisha serikali”.

Katika taarifa ya polisi iliyonakiliwa katika kituo cha polisi cha Muthithi kilichoko kaunti ndogo ya Kigumo, Bw Charles Muguro alidai kwamba alikuwa akipita karibu na kituo cha polisi cha Kambi ambapo afisa huyo alitokea gizani na akamshambulia.

Bw Muguro alionyesha ripoti za matibabu zikionyesha alivunjwa mikono yote miwili kando na kusababishiwa uvimbe usoni na sehemu nyingine mwilini.

“Mwanzoni afisa huyo alianza kunipiga akisema nilikuwa natembea nikiimba nyimbo za kitamaduni,” akasema.

Shambulio la aina hii limezua hisia kali miongoni mwa wenyeji kuhusu serikali na idara ya polisi eneo hilo.

Bw Simon Mwangi, 78, ambaye ni mwenyeji anasema kwamba “polisi kama huyu ni doa kubwa kwa utawala wa Rais William Ruto ambaye kila kuchao huwa anasisitiza kuhusu kutokubalika kwa udhalimu wa maafisa wa kiusalama”.

Alidai kwamba hii sio mara ya kwanza kwa maafisa katika kituo hicho cha Kambi kunaswa katika visa vya aibu lakini wakubwa wa kiusalama wa eneo hilo wakichangia pakubwa kuficha ukweli.

“Oktoba 2023 kuna afisa katika kituo hicho ambaye alinaswa na chifu wa Muthithi akisokota bangi ya kuuzia wenyeji ndani ya nyumba yake akiwa na mwanamke mshirika wa biashara ya mihadarati. Taarifa hii imfikie Kamanda wa polisi wa eneo la Kati Bi Lydia Ligami,” akasema.

Akaongeza: “Bi Ligami aulize maafisa wake wa Kigumo ilikuwa namna gani afisa huyo akafungiwa katika seli za polisi kwa wiki nzima lakini akaachiliwa na akarejeshwa kituoni kuendelea na biashara yake.”

Kamanda wa polisi wa Kigumo Bw Kiprono Tanui alithibitisha kuhusu masuala hayo akisema kwamba “nimeamrisha uchunguzi wa kina ufanywe na ukweli halisi ulio na ushahidi upatikane”.

Bw Tanui alisema kwamba hakuna afisa yeyote aliye na ruhusa ya kushambulia wananchi kwa msingi nje ya sheria “na nawahakikishia kwamba suala hili linachunguzwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za idara ya polisi”.

Bw Muthee Macharia ambaye ndiye kamanda wa polisi wa Muthithi ambapo Bw Muguro aliandikisha taarifa: OB: 21/14/12/2023.

Aliambia Taifa Jumapili kwamba “hili tukio linachunguzwa kwa uzito wa kisheria na taaluma ya polisi”.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alitaja tukio hilo kama la kusikitisha na ambalo linafaa kuchunguzwa hadi ukweli upatikane na iwapo madai hayo yatathibitishwa, hatua kali ichukuliwe maafisa wote husika”.

“Nimeshtuka kusikia kwamba afisa huyo anatuhumiwa kuwa pia mlanguzi wa mihadarati akitumia kituo cha polisi na wakubwa wake wanazubaa tu… Halafu isemwe kwamba alivamia mkazi akionekana wazi nia ilikuwa kumuua na bado wakubwa hao wamezubaa tu…

"Nitawagutusha kupitia kudai taarifa rasmi kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki iwapo katika kipindi cha wiki mbili hawatakuwa wamewajibikia ukora huo wa afisa mwenzao,” Bw Nyutu akasema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live