Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Papa atoa wito wapiganaji Sudan kuweka silaha chini

Afya Ya Papa Francis Yaimarika Baada Ya Kulazwa Hospitalini Usiku Papa atoa wito wapiganaji Sudan kuweka silaha chini

Mon, 17 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameeleza wasiwasi wake baada ya kuzuka kwa ghasia nchini Sudan ambapo watu wengi wameuawa na wengine kujeruhiwa wakati wanajeshi wa Serikali na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) wakipigania udhibiti wa taifa hilo.

Ghasia hizo zimeingia siku ya pili baada kuanza mapema jana Aprili 15 na taarifa kutoka muungano wa madaktari wa nchi hiyo zinasema tayari watu 56 wameshapoteza maisha na mamia kujeruhiwa, wakiwemo raia na wapiganaji.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Vatcan News inasema Papa amesema hayo wakati akiongea na umati wa waumini katika uwanja wa Mtakatifu Petro, na kuongeza kuwa anafuatilia kwa wasiwasi matukio yanayotokea Khartoum na kwingineko katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.

"Niko karibu na watu wa Sudan ambao tayari wamepitia mengi na natoa wito wa maombi, silaha ziwekwe chini ili mazungumzo yaweze kutawala kwa pamoja waweze kurudi kwenye njia ya amani na maelewano,” amesema Papa.

Ombi la Papa linakuja huku mapigano yakiripotiwa kuendelea katika mji mkuu wa nchi hiyo na katika maeneo mengine pia kufuatia kauli za pande zinazozozana kuwa haziko tayari kukomesha uhasama licha ya shinikizo la kidiplomasia linaloongezeka la kutaka kusitisha mapigano.

Mapigano hayo yamezuka baada ya miezi kadhaa ya mvutano mkubwa kati ya jeshi na kundi la RSF, kuchelewesha makubaliano na vyama vya kisiasa ili kuirejesha nchi katika kipindi cha mpito cha demokrasia, ambacho kilitoweka baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021.

Wakati huo huo, jumuiya ya madaktari ya ‘The Sudan Doctors Syndicate’ imetoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya kibinadamu na matibabu kusaidia vituo vya matibabu nchini humo.

Kundi hilo pia limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushinikiza pande zote mbili kuhakikisha zinaacha njia salama kwa magari ya wagonjwa na wafanyikazi wanaotoa matibabu.

Sudan ni nchi iliyo katika makutano ya Mashariki ya Kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara, inajulikana kwa historia yake ya mapinduzi ya kijeshi na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe tangu ilipopata uhuru wake miaka ya 1950.

Mzozo wa wenyewe kwa wenyewe uliodumu kwa muongo mmoja ulisababisha kugawanyika na kujitenga kwa Sudan Kusini mnamo mwaka 2011.

Chanzo: mwanachidigital