Kumekuwa na maoni mchanganyiko miongoni mwa Wasudan kuhusiana na hatma ya mapigano yanayoendelea kati ya majenerali wawili waliohasimiana. Huku baadhi yao wakiwa na matumaini huenda mapigano yakamalizika na wengine wakiwa wamepoteza matumani ya kurejea kwa amani katika taifa hilo la Afrika.
Wakizungumza na Sauti ya Amerika, baadhi ya Wasudan wameelezea imani yao kuwa juhudi za usuluhishi zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa zinaweza kuzaa matunda.
Mkurugenzi wa sera za uchumi kwa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Adam Elhiraika amesema ana imani kuwa vita hivyo vilivyozuka Aprili 15 vitamalizika kwa vile jeshi na vikosi vya dharura RSF havina uwezo wa kumudu kuendelea na mapigano kwa muda mrefu.
“Naamini kuwa vita hivi vitafikia mwisho. Pande mbili katika vita, RSF na jeshi la Sudan wanaonekana wamedhoofishwa na vita na hawadhani kuwa wana misuli ya kuendelea na vita hivi,” amesema Elhiraika.
Amesema vita hivi vimechochewa na waislamu ambao walitawala nchi tangu mwaka 1989, baada ya mapinduzi yaliyoongozwa na Omar Al Bashir ambaye naye alipinduliwa mwaka 2019, lakini kundi hilo la waislamu liliendelea kutawala taasisi za umma likiwemo jeshi.
“Ninaamini kwamba kwa kile ambacho wamekifanya na rekodi yao ya zaidi ya miaka 30 ya udikteta, si rahisi kwa kundi hilo la waislamu kurejea na kuidhibiti tena nchi,” amesema.
Moshi ukifuka juu ya majengo huko Khartoum, Mei 17, 2023. Picha na AFP. Moshi ukifuka juu ya majengo huko Khartoum, Mei 17, 2023. Picha na AFP. Kushindikana mara kwa mara kwa jitihada za kimataifa za kusitisha mapigano, kumewafanya baadhi ya Wasudan kupoteza matumaini ya kumalizika kwa mapigano ambayo yamesababisha madhara makubwa katika maisha ya raia na miundombinu.
Mwanaharakati wa haki za binaadamu Guy Yousif Adam kutoka Chuo kikuu cha Georgetown, hapa Marekani amesema kutokana na historia ya Sudan tangu mwaka 1956 ilipopata uhuru wake kutoka Uingereza, Sudan haijawahi kuwa na utawala wa kidemokrasia na huku serikali ikiwagawa Wasudan badala ya kuwaunganisha.
“Kihistoria Sudan haijawahi kutawaliwa kwa njia ambayo raia wameridhia, watu wamekuwa wakinyamazishwa kwa njia tofauti” alisema Guy, Na kuongeza kuwa “ Sina matumaini kama vita hii itamalizika katika siku za karibuni”
Naye mwandishi wa habari wa kijitegemea kutoka Sudan Fatma Gazali aliongeza “Sijui, ni vigumu kujua, mapigano yanaweza yakasambaa katika maeneo mengine”
Zikiwa zimepita zaidi ya siku 100 tangu mapigano hayo yazuke maelfu ya watu wamepoteza maisha, wakati nyumba nyingi na kambi za watu wasiokuwa na makazi zimechomwa moto na kuwa majivu, wakati takriban watu milioni 3.1 wameyakimbia makazi yao.