Kikosi cha wanajeshi wa Kenya, kimewasili katika mji wa Goma uliopo eneo la Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ili kushiriki operesheni ya pamoja inayolenga kupambana na waasi wa M23 katika eneo la mashariki la nchi hiyo.
Wanajeshi hao wapatao 100, waliwasili eneo hilo kwa Ndege mbili za Kenya na kutua katika uwanja wa ndege wa Goma hapo jana Jumamosi ya Novemba 12, 2022 na kulakiwa na viongozi wa eneo hilo.
Mara baada ya kuwasili, Luteni Kanali. Dennis Obiero wa Kenya aliwaambia waandishi wa habari kuwa lengo lililowafikisha hapo ni kuendesha operesheni kali pamoja na vikosi vya Kongo, na kusaidia kuwapokonya silaha wanamgambo.
Mapema Arpili, 2022, Viongozi wa jumuiya ya mataifa saba ya Afrika Mashariki, walikubaliana kuanzisha kikosi cha pamoja, ili kusaidia kurejesha usalama katika taifa la Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini.