Ongezeko la vyama vya siasa vinavyojiandikisha nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 limetajwa kuwa ni mradi wa viongozi wa vyama hivyo kwa ajili ya kujipatia kitita kikubwa cha fedha za walipakodi wa Kenya.
Ripoti zinasema, idadi kubwa ya vyama vya kisiasa vinavyosaka usajili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027 ni kiashiria cha jinsi mabilioni ya pesa ambazo vyama hivyo hupokea kutoka serikalini zilivyogeuza uendeshaji wa vyama vya kisiasa kuwa mradi wa biashara kubwa.
Vyombo vya Habari vya Kenya vinasema, msukumo huo wa kubuni vyama vipya vya kisiasa pia umechangiwa na mwenendo mbaya ulioko katika vyama vikuu vya kisiasa ambapo wakati mwingine wanasiasa hufanyiwa hiana na kunyimwa tiketi za kuwania nyadhifa za kisiasa.
Kufikia sasa stakabadhi kutoka Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), Anne Nderitu zinaonyesha kuwa, vyama 38 vipya vya siasa vimetuma maombi ya kutaka visajiliwe rasmi.
Aidha, vyama vingine 23 vimepata usajiliwa wa muda, hivyo kufanya idadi ya vyama vipya vya kisiasa nchini Kenya kuwa 90.
Inatazamiwa kuwa, huenda Kenya itakuwa na jumla ya vyama 151 vya siasa kufikia uchaguzi mkuu wa 2027.
Vyama vya siasa vimekuwa mradi wa kibiashara Kenya Stakabadhi za ORPP zimefichua jinsi vyama vinavyoongozwa na Rais William Ruto, rais mstaafu, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga vilivyotia kibindoni kiasi kikubwa cha fedha za Hazina ya Vyama vya Kisiasa (PPF) ndani ya miaka 10 iliyopita.
Sambamba na hayo, Rais William Ruto wa Kenya anashinikiza kuvunjwa vyama 13 tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza ili vijiunge na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).
Rais Ruto anasema, kuwepo kwa chama kimoja kikuu ndiko kutakakomuweka katika nafasi bora ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili mnamo 2027.